Akizungumza na waandishi wa habari jijini Tokyo, Katibu Mkuu amesema Umoja wa Mataifa unajivunia ushirikiano wake wa muda mrefu na Japan, akieleza kuwa nchi hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono amani, maendeleo na mshikamano wa kimataifa.
“Binadamu huwa na nguvu zaidi tunaposimama pamoja,” amesema Guterres, akiongeza kuwa ushirikiano ndio njia pekee ya kukabiliana na migogoro, mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa usawa duniani. Pia amesema mfumo wa sasa wa kifedha duniani hauzinufaishi vya kutosha nchi zinazoendelea ambazo zinaendelea “kuzama kwenye madeni na ukosefu wa fedha za maendeleo.”
Katibu Mkuu pia amesisitiza umuhimu wa kuipa sauti kubwa zaidi Afrika na nchi zinazoendelea ndani ya taasisi za kimataifa. “Tunahitaji mfumo wa kimataifa wenye haki zaidi na unaowapa uwakilishi mkubwa nchi zinazoendelea katika kushughulikia changamoto za dunia ya leo.”
Mambo mengine muhimu aliyozungumzia:
- Japan imekuwa mshirika wa Umoja wa Mataifa kwa miaka 70.
- Ushirikiano wa Japan na Afrika kupitia TICAD umetajwa kuwa mfano wa mafanikio ya ushirikiano wa maendeleo.
- Ametaka mageuzi ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuongeza uwakilishi wa Afrika na Amerika ya Kusini.
- Amesema benki za maendeleo duniani zinapaswa kuongeza msaada kwa nchi zinazoendelea.
- Ameonya kuhusu ongezeko la migogoro, gharama za maisha na athari za mabadiliko ya tabianchi duniani.
