Jamii ndio kitovu cha kukabili mlipuko wa Ebola DRC – WHOJamii ndio kitovu cha kukabili mlipuko wa Ebola DRC – WHO

Imani na ushiriki wa jamii vitakuwa msingi wa kuamua iwapo mlipuko wa hivi karibuni wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) utaweza kudhibitiwa, huku mamlaka za afya zikikimbizana kuzuia virusi kuenea zaidi na kuvuka mipaka.

Dkt. Marie Roseline Belizaire, Mkurugenzi wa Dharura katika Ofisi ya shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni (WHO) Kanda ya Afrika,amesema hayo katika mahojiano na Idhaa ya Kifaransa ya Umoja wa Mataifa wakati huu ambapo virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo vimeripotiwa DRC na Uganda.

Mkakati unaolenga jamii

Dkt. Belizaire amesisitiza mara kadhaa kuwa mwitikio wa kupambana na Ebola lazima ujengwe ndani ya jamii yenyewe badala ya kuletwa kutoka nje kwani, “kila dharura na kila mlipuko huanza katika jamii na kumalizwa na jamii.”

Kwa mujibu wa WHO, timu za mwitikio zinajumuisha wataalamu, vifaa vya matibabu na mifumo ya ufuatiliaji huku zikishirikiana na mamlaka za ndani pamoja na washirika wa kibinadamu. Lakini dkt. Belizaire ameonya kuwa hatua za kiufundi pekee hazitoshi.

“Hatuji kulazimisha sayansi yetu au kuziamuru jamii jinsi ya kuishi,” amesema, na kwamba “lazima tushirikiane na jamii ili kufanikisha mabadiliko ya tabia hatua kwa hatua kwa ajili ya kujilinda na kuokoa maisha.”

Hofu ya karantini husababisha wananchi kutoripoti wagonjwa

Mkakati huo unalenga kujenga imani kupitia viongozi wa jamii, kampeni za haraka za uhamasishaji na vituo vya matibabu vilivyo karibu na jamii zilizoathirika. 

WHO inasema uzoefu kutoka milipuko iliyopita umeonesha kuwa hofu ya kutengwa na familia mara nyingi huwazuia watu kuripoti dalili au kutafuta matibabu.

Kukabiliana na changamoto hiyo, Dkt. Belizaire amesema familia zitaruhusiwa kuwatembelea ndugu wanaopatiwa matibabu, huku msaada wa kisaikolojia na chakula pia ukiwa sehemu ya mwitikio huo.

Maeneo yenye mlipuko

Mlipuko huo umejikita katika majimbo ya mashariki ya Ituri na Kivu Kaskazini, ambapo maeneo 13 ya afya yameripoti maambukizi. Uganda pia imethibitisha wagonjwa wawili wanaohusishwa na mlipuko huo mjini Kampala, jambo linaloongeza hofu ya maambukizi kuvuka mipaka.

Hofu, taarifa potofu na unyanyapaa

Maafisa wa afya wana wasiwasi mkubwa kuhusu taarifa potofu na unyanyapaa unaohusishwa na Ebola, ambao unaweza kuwazuia watu walioambukizwa kujitokeza.

Afisa huyo wa WHO amehimiza jamii kuepuka uvumi na kutegemea taarifa rasmi za afya, akionya kuwa hofu na unyanyapaa vinaweza kudhoofisha juhudi za kufuatilia waliokutana na wagonjwa na kuwatenga waathirika kwa haraka.

“Watu walioathirika hawapaswi kunyanyapaliwa kwa sababu hilo linaweza kuwazuia kuripoti ugonjwa au kutafuta matibabu,” amsema.

WHO imewashauri wananchi kuripoti mara moja dalili kama homa, kutapika na uchovu mkali, kuepuka kugusana na majimaji ya mwili kutoka kwa wagonjwa au waliofariki, na kudumisha usafi wa mikono mara kwa mara.

Changamoto za usalama zinakwamisha mwitikio

Mlipuko huu unaendelea huku kukiwa na hali ya ukosefu wa usalama mashariki mwa DRC, ambako makundi yenye silaha, kuhama kwa wananchi na mazingira magumu vinatatiza shughuli za kibinadamu.

Dkt. Belizaire amesema uhamaji mkubwa wa watu unaohusishwa na maeneo ya uchimbaji madini pamoja na wakazi waliokimbia makazi yao unafanya iwe vigumu kufuatilia waliokutana na wagonjwa na kugundua visa mapema.

Hata hivyo, amesema WHO bado ina imani kuwa mbinu inayozingatia jamii inaweza kufanikiwa hata katika maeneo yenye migogoro. “Kwa kuzingatia uzoefu wa mwaka 2018 hadi 2020, milipuko katika eneo hili ilidhibitiwa,” amebainisha.

WHO na washirika wake, wakiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), pia wanafanya kazi kukabili changamoto za usafirishaji zinazosababishwa na miundombinu duni na njia ngumu za kufikika. Vifaa sasa vinasafirishwa kwa ndege hadi maeneo yaliyoathirika, yakiwemo Bunia jimboni Ituri.

Wasiwasi kuhusu aina ya Ebola isiyojulikana sana

Moja ya wasiwasi mkubwa kwa wanasayansi ni kwamba mlipuko huu unahusisha aina nadra ya Ebola ambayo haina chanjo iliyothibitishwa wala matibabu maalumu.

Dkt. Belizaire ameeleza kuwa aina hiyo iligunduliwa kwa mara ya kwanza Uganda mwaka 2007 na imewahi kusababisha milipuko miwili pekee kabla ya sasa.

“Hii si aina inayojulikana sana, iwe kwa jamii au kwa wanasayansi,” amesema.

Chanjo zilizopo sasa zilitengenezwa dhidi ya virusi vya Ebola aina ya Zaire, ambavyo ndivyo viliyosababisha mlipuko mkubwa Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016 pamoja na mlipuko wa DRC wa 2018 hadi 2020.

Kutokana na hali hiyo, jamii ambazo tayari zilichanjwa dhidi ya aina ya Zaire zinaweza kudhani kimakosa kuwa zinalindwa.

“Lazima tutafute njia sahihi ya kueleza kwa jamii kwamba chanjo waliyopewa mwaka 2018 hadi 2020 inawalinda dhidi ya aina hiyo pekee,” amesema Dkt. Belizaire.

WHO sasa imeanzisha mifumo yake ya utafiti na maendeleo ili kuchunguza uwezekano wa kutengeneza haraka chanjo inayolingana na aina hii mpya, ingawa maafisa wanaonya kuwa juhudi hizo bado ziko katika hatua za mwanzo.

Hatari ya kuenea zaidi

WHO imeonya kuwa mlipuko huo unaweza kugeuka kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa ikiwa maambukizi yataendelea kuvuka mipaka.

Dkt. Belizaire amesema hilo halimaanishi watu wanapaswa kuingiwa na hofu, bali mamlaka zinapaswa kuchukua hatua haraka na kwa uratibu.

“Kasi ya mwitikio katika siku za kwanza ni muhimu ili kukatiza maambukizi na kuzuia kuenea zaidi kwa mlipuko huu,” amesema.

Kwa sasa, WHO inasema vipaumbele vikuu ni kuimarisha ufuatiliaji, kugundua na kutenga visa haraka, kuwalinda wahudumu wa afya, kufuatilia waliokutana na wagonjwa, na kudumisha imani ya jamii zilizoathirika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *