
Russia imezindua mazoezi makubwa ya silaha za nyuklia yanayohusisha makumi ya maelfu ya wanajeshi, huku mapigano na Ukraine yakizidi kuwa makali na Rais Vladimir Putin akielekea China kwa ziara ya siku mbili.
Taarifa iliyotolewa na jeshi la Russia imesema manuva hayo yaliyoanza jana Jumanne, Mei 19 hadi 21, yanalenga kufanya mazoezi ya jinsi ya kupeleka na kutumia vikosi vya nyuklia “ikiwa kuna tishio la uchokozi.”
Mazoezi hayo yanafanyika baada ya kuvunjika mkataba wa New START, ukiwa mkataba wa mwisho wa silaha za nyuklia uliobaki kati ya Russia na Marekani, ambao ulimalizika rasmi mwezi Februari na kuondoa mipaka muhimu kwenye silaha za nyuklia za nchi hizo mbili.
Kwa mujibu wa Wizara ya Ulinzi ya Russia, mazoezi hayo yanahusisha zaidi ya wanajeshi 65,000, vifaa na zana za kijeshi 7,800, zaidi ya mitambo 200 ya kurushia makombora, pamoja na ndege, meli za kivita, manowari na nyambizi za nyuklia.
Russia pia itafanya majaribio ya makombora ya balestiki na ya cruise katika mazoezi hayo.
Wizara hiyo imeongeza kuwa mazoezi hayo yatajumuisha uratibu na Belarusi kuhusu “mafunzo ya pamoja na matumizi ya silaha za nyuklia zilizoko katika eneo la Jamhuri ya Belarusi.”
Russia tayari imeweka mfumo wake wa makombora wa Oreshnik wenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia huko Belarusi, mshirika wa karibu anayepakana na wanachama wa NATO. Tangazo hilo limetolewa saa chache kabla ya Putin kuondoka kwenda China.
Jumanne iliyopita, Putin alitangaza kwamba Russia ilikuwa imefanya majaribio ya kombora la kuvuka mabara la Sarmat lenye uwezo wa kubeba vichwa vya nyuklia, ambalo alilitaja kuwa ” kombora lenye nguvu zaidi duniani.”
