
Ripoti hiyo inaonesha kuwa fedha zinazotumwa na wahamiaji wanaoishi ughaibuni kwenda katika nchi za kipato cha chini na kati zilifikia makadirio ya dola bilioni 700 mwaka 2024, kiwango kilichopita misaada rasmi ya maendeleo pamoja na uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje kwa pamoja. Matokeo hayo yanaashiria mabadiliko makubwa katika namna misaada ya dharura na juhudi za uokoaji zinavyofadhiliwa duniani.
Mitandao ya diaspora yasafirisha msaada kwa haraka
Ripoti hiyo inaeleza kuwa jamii za wageni ughaibuni mara nyingi hujitokeza kwa haraka zaidi wakati wa majanga kwa kutumia mitandao ya kifamilia na kijamii inayowaamini wananchi ili kufikisha msaada moja kwa moja kwa waathirika.
“Jamii za diaspora ni miongoni mwa washirika wenye wepesi mkubwa na wanaoaminika zaidi katika kukabili majanga,” amesema Ugochi Daniels, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Operesheni wa IOM.
Amesema ushirikiano imara kati ya mashirika ya misaada na diaspora unaweza kuimarisha maandalizi, hatua na uokoaji wakati wa majanga.
Kuanzia Haiti hadi Ukraine, diaspora yajitokeza
Kupitia mifano kutoka Haiti, Lebanon, Ufilipino, Somalia na Ukraine, ripoti hiyo inaonesha jinsi mashirika ya diaspora yalivyokuwa mstari wa mbele kusaidia katika nyakati za dharura.
Nchini Ukraine pekee, diaspora ilikusanya dola milioni 283 katika mwaka wa kwanza wa vita, huku zaidi ya mashirika 100 ya diaspora yakijitokeza ndani ya siku chache baada ya tetemeko kubwa la ardhi la mwaka 2021 nchini Haiti. Imeongeza ripoti
Zaidi ya fedha, tahadhari na ujenzi wa mpya
Ripoti hiyo inaeleza kuwa mchango wa diaspora hauishii kwenye fedha pekee. Jamii hizo zimechangia kuanzishwa kwa mifumo ya tahadhari za mapema, kuboresha huduma za afya na makazi salama, pamoja na kusaidia juhudi za ujenzi wa upya zinazoongozwa na jamii zenyewe.
Aidha, diaspora huleta uelewa wa tamaduni, maarifa ya mazingira ya eneo husika na njia za mawasiliano zinazoaminika ambazo zinaweza kuimarisha utoaji wa misaada kwa watu walio hatarini zaidi.
IOM yataka ushirikiano wa kudumu
IOM sasa inazitaka serikali, wafadhili na mashirika ya misaada kubadili ushirikiano wa muda mfupi na kuanzisha mifumo rasmi ya kufanya kazi pamoja na jamii za diaspora.
Ripoti hiyo inapendekeza kuwepo kwa mifumo rahisi ya ufadhili, zana za kidijitali za uratibu, ushirikiano bora wa takwimu na programu maalum za kujenga uwezo ili kutumia kikamilifu nguvu ya diaspora katika kukabili majanga.
Matokeo hayo pia yatachangia maandalizi ya Mkakati mpya wa Diaspora wa IOM ambao unalenga kufanya ushirikiano na diaspora kuwa nguzo kuu ya kazi za shirika hilo duniani.
