
UONGOZI wa Junguni United yenye maskani yake Wete kisiwani Pemba, umetangaza kumvua madaraka Suleiman Mwidani Asaa nafasi ya katibu mkuu wa klabu hiyo kwa tuhuma za kutumia fedha za timu kwa masilahi yake binafsi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Meneja wa Junguni United, Hamad Abdalla Khalfani amesema uamuzi huo umetoka baada ya kikao kilichofanyika Mei 19, 2026, kilichohusisha viongozi wa timu hiyo akiwemo mshika fedha, Khamis Kombo Mussa.
Amesema wamefikia uamuzi wa kumvua madaraka hayo baada ya kutoridhishwa na vitendo vyake vinavyokiuka maadili ya klabu.
“Kwa pamoja klabu imeamua rasmi kukuachisha nafasi yako ya ukatibu kuanzia tarehe ya barua hii (Mei 19, 2026), hivyo unatakiwa yale yote ambayo unayamiliki ikiwa ni mali ya klabu uyarudishe kwa uongozi husika wa klabu. Klabu inakushukuru kwa kuwa pamoja muda wote huo na kukutakia mapumziko mazuri,” ilieleza sehemu ya barua hiyo ambayo nakala yake imetumwa kwa mhusika, Mrajisi wa Vyama vya Michezo Zanzibar na Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF).
Meneja huyo amesema licha ya Junguni United kushuka daraja, bado wana matumaini ya kurudi tena msimu ujao, ndiyo maana wameanza kuwaweka pembeni viongozi wanaoonekana hawapo njia sahihi huku wakitafuta walio imara.
Akitoa ufafanuzi wa hilo, Mwidani alikiri kupokea taarifa hiyo huku akisisitiza, waliofanya hivyo hawana mamlaka ya kumvua majukumu yake.
“Wamefanya vitu ambavyo havina utaratibu kwa sababu nilichaguliwa kwa kura, hawawezi kuniondosha kwa namna hiyo na hawahusiki kufanya uamuzi wa aina hiyo kwani wao ni waajiriwa na sio waajiri,” amesema kiongozi huyo.
Mwanaspoti lilimtafuta Naibu Katibu Mkuu wa ZFF, kisiwani Pemba, Khamis Juma na amesema yeye kama kiongozi mwenye dhamana, amebariki uamuzi huo.
“Barua hiyo nimeiona na nimebariki kwani imefuata kanuni na wenye mamlaka ya kumfukuza kiongozi ni uongozi wa timu,” amesema.
Ikumbukwe, hayo yanajiri baada ya Aprili 27, 2026 Mwanaspoti kutoa taarifa za hali mbaya kiuchumi inayopitia Junguni United kiasi cha kuwafanya wachezaji wa kikosi hicho kufika msikitini kuomba msaada wa kifedha huku msemaji wa timu hiyo, Suleiman Sultan Hemed akikiri kukwama kwao kujiendesha kulitokana na ukosefu wa fedha ilihali walishapokea fungu kutoka kwa mdhamini mkuu wa Ligi Kuu Zanzibar.
