Dar es Salaam. Wakati Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikisimulia tukio la ‘kutekwa’ kwa David Djumbe ambaye ni msaidizi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, Jeshi la Polisi limesema linafuatilia tukio hilo.
Djumbe anadaiwa kuchukuliwa nyumbani kwake Mabwepande, Bunju jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo Alhamisi, Mei 21, 2026 kisha akarejea nyumbani kwake akiwa na pingu mikononi na kuvuja damu.
Mbali na pingu aliyofungwa mikononi, alikuwa na majeraha mbalimbali mwili mwake. Baadaye, Djumbe akiwa na wanafamilia na baadhi ya viongozi wa Chadema walikwenda Kituo cha Polisi Osterbay kwa ajili ya kufunguliwa pingu hizo.
Hadi saa kumi Djumbe alikuwa bado kituoni hapo akitoa maelezo.
David Jumbe akiwa na pingu akiripoti kituo cha Polisi Osterbay Dar es Salaam
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, Amani Golugwa ndiye amesimulia tukio hilo mbele ya waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho, Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Kabla ya Golugwa kuzungumza na waandishi wa habari, askari polisi walitanda kwenye viunga vya makao makuu hayo ya Chadema wakifanya doria huku wengine wakiwa ndani ya ofisi hiyo wakimhoji kiongozi huyo juu ya suala hilo la Djumbe.
Mkutano huo na waandishi ulikuwa ufanyike saa 3 asubuhi lakini uliofanyika saa 5 kutokana na mahojiano hayo na polisi.
Golugwa amesema alikuwa akihojiwa na askari waliojitambulisha wametoka Kituo cha Osterbay na wanamtaka Djumbe, aliyedhaniwa yupo kwenye ofisi za chama hicho.
Amesema walipokea taarifa ya kutekwa kwa mwanachama huyo na msaidizi wa Lissu akiwa kwenye gari na rafiki yake, Allan Macha, walizuiwa na gari dogo aina ya Toyota Probox na pikipiki mbili, kisha watu sita wakashuka.
Miongoni mwa watu hao kwa mujibu wa Golugwa alikuwepo mtu aliyevaa sare ya Polisi na wengine wakiwa na nguo za kiraia.
“Watu hao walijitambulisha ni Polisi lakini walifanya tendo la kiharamia, baada ya kuvamia gari alilokuwa amepanda Djumbe na rafiki yake na kutokomea naye kuelekea eneo la Mbweni,” amesema.
Macha, rafiki wa Djumbe amesema kabla ya tukio hilo rafiki yake huyo alimpigia simu ampitie warudi nyumbani pamoja kwa kuwa gari lake lilikuwa limepata hitilafu.
Baada ya kumchukua wakati tunaelekea nyumbani, umbali mfupi kutoka nyumbani kwa Djumbe waliona gari linawafuatia likiwa kwenye mwendokasi huku kukiwa na pikipiki mbili.
“Mimi ndiyo niliona gari na nilikuwa nimemwomba Djumbe aendeshe gari kwa kuwa naumwa, hivyo nilipoona hali ile nilimuuliza kama analiona gari hilo, basi tukashauriana tulipishe kwa kuwa njia ni nyembamba sana,” amedai.
Macha amedai baada ya kulipisha gari hilo liliwazuia kwa mbele na walipojaribu kujinasua waliendelea kuwazuia na hapo wakatafuta mbinu ya kukimbilia eneo lenye watu kwa usalama zaidi.
“Watu wale walishuka wakiwa sita na kwa kuwa hatukufunga gari walikuja na kujitambulisha ni askari na wakatuweka chini ya ulinzi, nilichokuwa nashuhudia ni kama naangalia filamu,” amedai.
“Wakati wakisema mpo chini ya ulinzi, Djumbe alihoji tupo chini ya ulinzi kwa sababu gani, kitendo cha kuuliza waligawanyika na kumtoa Djumbe kwenye gari na mimi pia, nilianza kupiga kelele watekaji watekaji,” amesimulia Macha.
Baada ya sauti ya Macha iliyokuwa ikiomba msaada, walijitokeza madereva bodaboda ambao walikuwa wakirudi nyumbani na hapo watu hao waliodaiwa ni watekaji waliwachukua watu hao na kuanza kukimbia akiwa na Djumbe.
Macha amesema wakati huo watuhumiwa hao wa utekaji wakikimbia, bodaboda walianza kuwakimbiza na hapo Macha akaanza kumpigia simu rafiki yake mwingine, akiomba msaada na watu hao kuzuiwa kwa mbele.
“Lengo langu ni kuzuia gari langu, tulikwenda kwa kasi na pikipiki na kulipita gari lililombeba Jumbe, sisi tulitaka kulizuia gari la mbele ambalo lilikuwa na kasi kubwa sana,” amesema.
Amesema baada ya kufikia eneo lililowekwa vizuizi madereva bodaboda walianza kupunguza mwendo na hapo alianza kupiga kelele za utekaji, utekaji na bodaboda waliendelea kuongezeka.
Amesema baada ya watekaji kufika eneo lenye kizuizi walikigonga na kuelekea Bunju huku akifukuzwa na madereva bodaboda.
Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu, David Jumbe akitoka kituo cha Polisi Osterbay Dar es Salaam kutoa maelezo ya tukio la utekaji dhidi yake.
“Walipofika njia ya kuelekea Mbweni waliona bodaboda wanaongezeka, ndipo walianza kufyatua risasi juu,” amesema.
Hata hivyo, kelele za risasi hazikuwashtua bodaboda hao, waliendelea kuwafukuza hadi eneo la msituni, walipofika kwenye kizuizi kingine walipunguza kasi na kusimamisha gari na kushuka wote.
Muda mfupi baada ya watu hao kushuka, wakafyatua risasi nyingi kwa mara nyingine na madereva hao wakanza kutawanyika.
“Kilichotokea baada ya milio ya risasi kutulia, bodaboda walishauri tumpigie OCD ambaye sikujua ni wa eneo gani na nikapewa simu nikamwelezea kilichotokea,” amesema.
Macha amedai alishauriwa kuripoti polisi akaenda kituo cha jirani na walipokuwa ambapo aliwakuta askari wanne, wawili wakiwa nje.
Alipofika eneo la mapokezi na kueleza uhalisia wa tukio hilo, askari walimwambia asubiri, kisha wakasema tukio hilo limetokea Kibaha hivyo warudi wakaripoti Polisi Mapinga,” amedai.
Macha amedai baada ya kufuata ushauri huo na kwenda Polisi Mapinga askari aliyekuwa eneo la mapokezi alimwambia haiwezekani mtu huyo (Djumbe) achukuliwe peke yake lakini yeye akabaki.
Baadaye alielezwa gari lake limetelekezwa Mbweni na kuwa kamanda aliyezungumza naye alikuwa ametoa maelekezo lipelekwe Kituo cha Polisi Mbweni.
“Nikaomba kumuuliza afande kwenye gari langu nilikuwa na kompyuta mpakato na Sh800,000, na je nitavipata? Akaniambia hawezi kunihakikishia kwamba nitavipata,” amesema.
Simulizi ya Djumbe
Katika kipande cha video cha Djumbe kilichosambaa mitandaoni, mbali na kueleza tukio hilo kama alivyoeleza rafiki yake Macha, anasimulia jinsi alivyonusurika.
“Hizi damu walikuwa wananipiga kichwani na kitako cha bunduki huku wanasema ‘leo ndiyo siku yako ya mwisho’ na mimi nikiwa najaribu kupambana nao. Kwa kuwa walikuwa wameshanifunga pingu ikawa vigumu kukabiliana nao,” anadai.
“Sasa wakati tunakwenda kutokana na ubovu wa barabara gari likawa linakimbia likiruka sana, pingu zikawa zinakaza sana. Nilikuwa nahisi mikono inataka kukatika. Nikasikia wanajadili kuwa bodaboda wanatufuatilia na wanaendelea kuongezeka. Nilikuwa kwenye buti ya Probox na nilikuwa nahangaika kufungua lakini hazifunguki na
Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu aliyenusurika kutekwa David Djumbe akitoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala baada ya kufanyiwa matibabu.
walikuwa wamenikanyaga pia.”
“Walivyoona bodaboda wanaongezeka wakawa wanaelekezana twende Kituo cha Polisi Mbweni, mwingine akasema hapana bosi kasema huyu hatakiwi kufikishwa polisi.”
“Sasa wakati wanakwenda wakajikuta wamefika msituni pale Mbweni, wakashuka wote kwenye gari na kuanza kupiga risasi bodaboda wasiendelee kuwafuata huku wakiamini mimi siwezi kunyanyuka kwenye buti,” anadai.
“Nilivyoona wameshuka nikajirusha kwenye siti ya katikati, nikafungua loki nikaitoa, nikashuka upande wa msitu nikaingia msituni, wakati wanarudi kwenye gari mimi nimeshaingia msituni.”
“Wakaanza kunifuatilia wakipiga risasi msituni na msitu ukiwa umefunga sana hawawezi kupita. Nami nikiwa natambaa kwenye miiba na suruali yangu ilinasa kwenye miiba nikaiacha huko nikatambaa kwa muda wa saa moja na nusu, ndipo nikaweza kutoka upande wa pili.”
“Na nilikuwa na hela Sh700,000 za kuwalipa mafundi waliokuwa wanatengeneza gari langu lilikuwa gereji, lakini wameninyang’anya hela zangu,” amedai.
Kauli ya Polisi
Kufuatia tukio hilo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imetoa taarifa kwa umma ikisema tangu jana Mei 20, 2026 usiku wamekuwa wakifuatilia taarifa zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii kuwa David Djumbe alikamatwa na watu ambao hawakujitambulisha huko maeneo ya Bunju.
Taarifa hiyo ya Polisi iliyotolewa na Kaimu Kamanda wa Kanda hiyo, Faustine Mafwele imeeleza kuwa katika ufuatiliaji wamefanikiwa kupata gari aina ya Toyota Wish rangi nyeusi ambalo ni mali ya Allan Macha, ambalo Djumbe alikuwa amepanda.
Mafwele amesema leo Mei 21 asubuhi wamepokea taarifa kuwa yupo katika Ofisi za Chadema Mikocheni. Askari polisi walifika katika ofisi hizo lakini hawakumkuta bali aliyekuwepo ni mtu ambaye inadaiwa alikuwa naye wakati anakamatwa.
Aidha, Djumbe ameshapatikana na uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini ni watu gani waliomkamata na kwa madhumuni gani ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.
