Mkuu wa WHO ataka hatua za haraka dhidi ya Ebola huku wagonjwa wapya watatu wa Ebola wakithibitishwa UgandaMkuu wa WHO ataka hatua za haraka dhidi ya Ebola huku wagonjwa wapya watatu wa Ebola wakithibitishwa Uganda

Akizungumza na Mawaziri, wanadiplomasia na wataalamu wa afya mjini Geneva, Uswisi mwishoni mwa mkutano huo wa wiki nzima, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema kuwa milipuko ya hivi karibuni ya Ebola na virusi vya Hanta inaonesha kuwa dunia bado iko katika hatari ya magonjwa ya kuambukiza yanayosambaa kwa kasi. 

Amesisitiza umuhimu wa kukamilisha kiambatisho cha PABS chini ya Mkataba wa Janga la Magonjwa (Pandemic Agreement), amba oni mfumo muhimu wa upatikanaji wa vimelea vya magonjwa na mgawanyo wa manufaa.

Mgonjwa mmoja ametoka DRC kusaka tiba Uganda

Wito wake umetolewa wakati Uganda imethibitisha leo  Jumamosi wagonjwa wapya watatu wa Ebola wa virusi aina ya Bundibugyo ambavyo hadi sasa havina tiba wala chanjo.

Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa X, zamani Twitter, Dkt. Tedros amesema kuwa wagonjwa hao ni pamoja na mhudumu wa afya kutoka Uganda, dereva mmoja na raia mmoja wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) aliyesafiri kutoka Jimbo la Ituri kwenda Uganda kupata matibabu.

“Hii inafanya jumla ya watu waliopatikana na ugonjwa wa Ebola unaosababishwa na virusi vya Bundibugyo nchini Uganda kufikia watano,” amesema.

Amepongeza Wizara ya Afya ya Uganda kwa juhudi zake za kugundua, kufuatilia na kuwahudumia watu wanaoshukiwa au kuthibitishwa kuambukizwa Ebola. Amesema katika kipindi hiki muhimu cha kukabiliana na mlipuko huo, ni lazima mamlaka kuendelea kuwa makini ili kudhibiti kusambaa kwa virusi hivyo.

Dkt. Tedros amesema WHO kwa kushirikiana na Kituo cha Afrika cha Kudhibiti Magonjwa (Africa CDC) pamoja na washirika wengine nchini DRC na Uganda wanafanya kazi kwa karibu kudhibiti mlipuko huo, kusaidia waathirika na kuimarisha mwitikio wa pamoja.

Mlipuko wa hivi karibuni wa Ebola uliripotiwa kwa mara ya kwanza nchini DRC Jumamosi iliyopita kabla ya visa kuripotiwa pia Uganda.

Ijumaa, WHO iliongeza kiwango cha tathmini ya hatari ya taifa kwa DRC hadi “juu sana”, ingawa hatari ya kimataifa bado imeendelea kuwa “ndogo”.

Juhudi za mipakani kudhibiti mlipuko wa Ebola

Mjini Kampala, Uganda, WHO iliandaa mkutano wa siku mbili wa ngazi ya juu wa mawaziri kuhusu uratibu wa mipakani katika kukabiliana na mlipuko wa Ebola ya Bundibugyo.

Akihutubia mawaziri kutoka Sudan Kusini, DRC na Uganda, Dkt. Marie Roseline Belizaire, Mkurugenzi wa WHO Afrika wa Maandalizi na Mwitikio wa Dharura, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha na kudumisha ushirikiano wa mipakani ili kudhibiti mlipuko huo.

Ameonya kuwa ucheleweshaji wa mwitikio unaweza kuwa na madhara makubwa na kusisitiza kuwa mifumo imara ya ufuatiliaji na maandalizi ni muhimu kwa sababu “wakati huokoa maisha” wakati wa milipuko.

Milipuko ya Ebola na virusi vingine yaonesha hatari za kimataifa

Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema milipuko inayoendelea inaonesha wazi kuwa virusi havitambui mipaka ya kitaifa, akisisitiza kauli zilizotolewa wakati wa mkutano huo kuwa usalama wa afya duniani unategemea hatua za pamoja.

Timu za WHO zilisifiwa kwa kazi yao mstari wa mbele katika kukabiliana na milipuko ya Ebola na hantavirus huku zikisaidia pia mifumo ya afya katika nchi mbalimbali duniani.

Mkutano huo ulisikia wito wa mara kwa mara kwa nchi kushirikiana kupitia taasisi za kimataifa badala ya kukabiliana na vitisho vya afya kila nchi kivyake.

Makubaliano muhimu yaliyofikiwa katika mkutano huo

Mkutano wa wiki moja umehitimishwa kwa nchi wanachama kupitisha maazimio kuhusu vipaumbele mbalimbali vya afya, ikiwa ni pamoja na:

  • Kudhibiti kifua kikuu
  • Huduma za dharura na wagonjwa mahututi
  • Tiba mahsusi 
  • Kuzuia na kutibu kiharusi
  • Magonjwa ya kitropiki yaliyopuuzwa (NTDs)
  • Upigaji picha za uchunguzi wa magonjwa
  • Usalama wa matumizi ya dawa
  • Upandikizaji wa viungo na magonjwa ya ini

Nchi pia zimekubaliana kufanya mageuzi ya mfumo wa afya duniani kupitia mchakato unaoongozwa na nchi wanachama chini ya uratibu wa WHO ili kuboresha ushirikiano wa kimataifa wakati wa migogoro ya afya.

Viongozi wamesisitiza kuwa mafanikio ya makubaliano hayo yatategemea utekelezaji katika ngazi ya nchi, ikiwemo kuimarisha mifumo ya afya, upatikanaji wa fedha na ushirikishwaji wa jamii.

Mwelekeo wa baadaye kwa nchi wanachama wa WHO

Baraza la Afya la WHO limeeleza vipaumbele kadhaa kwa nchi wanachama katika siku zijazo:

  • Kukamilisha na kutekeleza Mkataba wa Janga la Magonjwa pamoja na kiambatisho cha PABS
  • Kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na mwitikio wa haraka kwa milipuko
  • Kuwekeza katika mifumo imara ya afya ya kitaifa
  • Kuboresha upatikanaji wa chanjo na huduma za afya
  • Kuongeza ufadhili endelevu kwa shughuli za WHO
  • Kupanua ushirikiano wa kimataifa na kubadilishana taarifa

Mchango endelevu wa kifedha

Mkurugenzi Mkuu wa WHO pia amezitaka nchi wanachama kuendelea kuongeza michango yao ya kifedha ili kuhakikisha WHO inaendelea kuwa taasisi imara, huru na yenye uwezo wa kukabiliana na dharura za afya duniani siku zijazo.

Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa makubaliano ya kimataifa lazima yatafsiriwe kuwa hatua halisi zinazolinda jamii, kudhibiti milipuko kwa haraka na kuhakikisha huduma za afya zinawafikia watu walio hatarini zaidi.

“Kila taifa linakuwa na afya bora na salama zaidi pale mataifa yote yanapokuwa na afya bora na salama zaidi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *