
Rais Masoud Pezeshkian anasema wataalamu wa mahusiano ya umma wanapaswa kuchukua jukumu muhimu katika kuongeza uelewa wa umma, ikizingatiwa kwamba vyombo vya habari vya Kizayuni vinawazuia watu kuona na kujua ukweli.
Rais Pezeshkian amesema: “Leo, baadhi ya vyombo vya habari viko mikononi mwa Wazayuni na haviruhusu watu kuona ukweli. Lakini kwa zana zilizopo na mtandao wa kijamii, mahusiano ya umma yanaweza kuimarisha na kupanua ushawishi huu na kuongeza kiwango cha ufahamu.”
“Huu ni wajibu mkubwa unaowakabili wataalamu wa mahusiano ya umma,” amesema Rais Pezeshkian akiiambia hadhira ya maafisa wa mawasiliano.
Matamshi ya Rais yanakuja huku kukiwa na ushahidi mkubwa kwamba utawala wa Israel unafanya mojawapo ya ukandamizaji mkubwa zaidi wa vyombo vya habari katika historia ya utawala huo, ukificha kimfumo athari kamili za mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran na vipigo vya Hizbullah dhidi ya utawala huo.
Mnamo Machi 11, wakati ripoti za shambulio kubwa la makombora ya ya Iran na Hizbullah zilipoibuka, waandishi wa habari wa Israel walichunguza suala hilo na kugundua kuwa taarifa hiyo ni ya kuaminika — lakini mkaguzi wa kijeshi alizuia uchapishaji wa taarifa hiyo.
Vilevile picha mpya za satelaiti zilizochambuliwa zimefichua uharibifu na hasara kubwa katika vituo vingi vya kijeshi vya Israel kufuatia mashambulizi na operesheni za kujihami za Iran na harakati ya Lebanon Hizbullah na hivyo kuzusha maswali kuhusu ukubwa wa uharibifu ambao Tel Aviv inaweza kuuficha mbele ya umma.
Picha mpya zilizonukuliwa na Yedioth Ahronoth zinaonyesha athari za mashambulizi ya Iran na Hizbullah kwenye Kituo cha Anga cha Ramat David, Kituo cha Anga cha Nevatim, kituo cha ujasusi cha Mishar, na Kambi ya Shimshon, ambapo moto mkubwa ulienea mamia ya mita baada ya mashambulio hayo.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa picha zenye ubora wa chini zilitumika kimakusudi, na hivyo “kuzidisha shaka kuhusu uwazi wa utawala wa Kizayuni kuhusu kiwango halisi cha uharibifu uliofanywa na mashambulizi ya Iran na Hizbullah.”
Hata hivyo, Rais Pezeshkian amesifu ufanisi wa chombo cha uhusiano wa umma cha Iran, akisisitiza wajibu wake wa kupanua ushawishi zaidi nje ya mipaka ya kitaifa.
