
Dar es Salaam. Somo hili ni mahususi kwa wale wote wenye ndoto ya kuwa na ndoa zenye mafanikio na utulivu.
Kama huna mpango wa kufunga ndoa, huenda maudhui haya yasikufae kwa sasa, lakini kama unatazamia kuingia kwenye maisha ya mume na mke, basi misingi hii ni kwa ajili yako.
Watu wengi wamekuwa wakifundishwa na kuelewa kwamba kitu pekee kinachohitajika ili kuishi kwenye ndoa ni upendo pekee.
Dhana kwamba upendo ukishakuwepo basi mengine yatajipa yenyewe, ni nadharia potofu ambayo imewaingiza wengi kwenye matatizo makubwa. Ukweli ni kwamba kuna nguzo nyingine muhimu zinazopaswa kushirikiana na upendo ili kuidumisha ndoa au uhusiano.
Msingi wa kwanza ni ufahamu mkubwa. Ndoa imara hujengwa kwa kufahamu sababu hasa ya ninyi kuwa pamoja na kuelewa mambo ya kuzingatia, mambo gani ya kufanya na nini uepuke.
Ni muhimu kujiuliza unamfahamu mwenzako kwa kiasi gani na una uelewa gani kuhusu matarajio ya jinsi yake.
Sambamba na ufahamu, uelewa ni busara nyingine inayopaswa kuwepo kabla ya kufunga ndoa.
Unapaswa kuelewa tabia ya rafiki yako, nguvu zake na udhaifu wake. Kuna mambo mengi kwenye ndoa hayahitaji majibizano bali yanahitaji uelewa tu wa haraka ili kupunguza misuguano isiyo ya lazima.
Usipoelewa, ni vyema kuuliza kuliko kujifanya unaelewa wakati moyoni una mashaka.
Hekima inasimama kama nguzo ya tatu muhimu. Hii ndiyo inayokuwezesha kufanya uamuzi sahihi kwa ajili ya ustawi wa ndoa yako bila kuleta majuto hapo baadaye.
Hekima inakusaidia kutumia uelewa na ufahamu wako vizuri. Jambo la kushangaza ni kwamba mapenzi au upendo unapaswa kuwa jambo la nne na si la kwanza.
Unapokuwa na uelewa, ufahamu na hekima, basi upendo unakuja kuketi sehemu salama. Bila nguzo hizo tatu, upendo pekee utashindwa kuzuia misuguano isiyoisha.
Maswali ya kujiuliza
Kabla ya kuingia kwenye ndoa, ni vyema ukajiuliza kwanini unafanya hivyo na ni sababu zipi zinakusukuma.
Kupata majibu ya kiufasaha mapema kutakuepusha na maswali ya majuto baada ya kuoa au kuolewa, kwani wakati huo unaweza kuwa umeshalala na itakuwa umechelewa mno kufanya marekebisho ya msingi.
Ili kufikia kilele cha mafanikio, unahitaji kupita katika ngazi kuu mbili za uhusiano. Ngazi ya kwanza na yenye umuhimu mkubwa kuliko zote ni uhusiano wako na Muumba.
Ngazi hii ndiyo inayoamua kiasi kikubwa cha uhusiano wako na watu wengine. Kumshirikisha Mungu katika kila tamanio la moyo wako, kuanzia aina ya mume au mke unayemtaka hadi sifa za familia unayoota, ni hatua ya usalama. Wengi hukurupuka na kusahau ngazi hii, kisha hujikuta kwenye ndoa ambazo si ndoto yao. Tafiti zinaonyesha kuwa wanandoa wenye uhusiano mzuri na Muumba wao huweza kuthaminiana na kuheshimiana kwa urahisi zaidi. Kumbuka kuwa unaweza kuoa au kuolewa wakati wowote, lakini huwezi kuoa au kuolewa na kila mtu.
Ngazi ya pili ya uhusiano ni familia. Huwezi kumtenganisha mchumba na familia yake, hivyo uhusiano wa familia wenye nguvu unakusaidia kufanya uamuzi mzuri.
Ni bora ukaingia kwenye maumivu ya kugundua mambo magumu kabla ya ndoa kuliko kuvinyamazia na kuja kupata maumivu makali zaidi ukiwa ndani ya ndoa tayari.
Ni wajibu wako kuifahamu familia ya mpenzi wako kwa kina. Jua uhusiano wake na wazazi wake, ndugu zake, na hata historia ya magonjwa ya kurithi au tabia za kifamilia.
Chunguza imani zao na jinsi wanavyoshirikiana. Taarifa hizi ni nyenzo muhimu huko mbele kwa sababu mpenzi unayemchagua anaweza kuwa na matokeo chanya au hasi katika uhusiano wako na familia yako mwenyewe.
Kuwa makini, kwani baadhi ya migogoro huisha baada ya ndoa, lakini mingine ndiyo kwanza huanza pale tu mnapokula kiapo.
