
Kufuatia ripoti kwamba baadhi ya ndege za abiria kutoka barani Afrika zimezuia kuingia Marekani kutokana na mlipuko wa Ebola, shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Anga, ICAO limesema usafiri wa anga wa kimataifa unaendelea kuwa salama licha ya kutangazwa kwa mlipuko huo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, (DRC) na Uganda.
Katika taarifa yake iliyotolewa 25 Mei huko Montreal nchini Canada, shirika hilo limetoa wito kwa serikali, mashirika ya ndege, na mamlaka za viwanja vya ndege kufuata kikamilifu mapendekezo ya WHO yanayotegemea ushahidi ili kuhakikisha sekta ya anga inaendelea kufanya kazi kwa usalama na ufanisi duniani kote.
Kwa nini ICAO inasema usafiri wa anga bado ni salama
Msimamo wa ICAO unategemea mambo mawili muhimu:
- Asili ya virusi vya Bundibugyo, ambavyo havisambai kupitia hewa wala kwa mgusano wa kawaida.
- Mfumo ulioboreshwa wa kimataifa wa afya katika sekta ya anga uliojengwa baada ya janga la COVID‑19.
ICAO imeeleza kuwa virusi aina ya Bundibugyo vinavyosababisha mlipuko wa sasa vinahitaji mgusano wa moja kwa moja na majimaji ya mwili ili kusambaa — njia ya maambukizi inayofanya uwezekano wa maambukizi ndani ya ndege kuwa mdogo sana.
Tathmini hii ya kisayansi kutoka WHO ndiyo msingi wa uthibitisho wa ICAO kwamba huduma za usafiri wa anga zinaweza kuendelea bila kufungwa kwa mipaka au marufuku za safari.
Hivi sasa sekta ya anga iko vema zaidi kuliko wakati wa COVID-19
Wakati huohuo, ICAO imesisitiza kuwa sekta ya anga sasa imejiandaa vizuri zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya 2020 wakati wa mlipuko wa coronavirus“>COVID-19.
Shirika hilo linasema kiambatanisho cha 9 cha Mkataba wa Kimataifa wa Usafiri wa Anga sasa kina sura maalum kuhusu masharti ya kiafya, yakisaidiwa na mwongozo uliosasishwa katika Mwongozo wa Uwezeshaji wa ICAO (Doc 9957).
Viwango hivi vinahakikisha utoaji wa taarifa kwa haraka na kwa muundo mmoja kati ya nchi, mashirika ya ndege, viwanja vya ndege, na taasisi za afya.
Zana za kidijitali — mathalani, tamko la afya kwa njia ya kielektroniki, mchakato wa kuvuka mipaka bila kugusa vifaa, na ubadilishanaji wa taarifa kiotomatiki — zimejumuishwa katika mapendekezo ya ICAO ili kusaidia nchi kugundua na kudhibiti hatari za kiafya kwa ufanisi zaidi.
Kupitia Mpango wa Ushirikiano wa Kuzuia na Kusimamia Matukio ya Afya ya Umma katika Usafiri wa Anga (CAPSCA), ICAO inaendelea kushirikiana kwa karibu na WHO na mamlaka za kitaifa kutoa hatua za kupunguza hatari zinazotegemea ushahidi.
Nini mashirika ya ndege na mamlaka za anga zinapaswa kufanya
ICAO inahimiza wadau wa sekta ya anga kuzingatia mapendekezo ya muda ya WHO. Matarajio muhimu ni pamoja na:
- Kufuata kwa ukamilifu taratibu za afya za WHO — Mashirika ya ndege yahakikishe wahudumu na wafanyakazi wa ardhini wanafuata taratibu za kuzuia maambukizi, hasa wanapohudumia abiria wagonjwa au safari za uokoaji wa kitabibu.
- Kusaidia uchunguzi wa kiafya wa kuondoka katika nchi zilizoathirika — DRC na Uganda zinapaswa kuwapima kablaya safari wasafiri wenye homa isiyoelezeka au dalili zinazofanana na Ebola inayosababishwa na virusi vya Bundibugyo.
- Kuepuka vizuizi visivyo vya lazima vya usafiri — ICAO imesisitiza mwongozo wa WHO kwamba nchi hazipaswi kufunga mipaka au kuweka marufuku za safari, kwani hatua hizo hazina ufanisi na zinaweza kuathiri juhudi za kudhibiti mlipuko.
- Kuhakikisha wagonjwa waliothibitishwa na waliokaribiana nao hawasafiri — Isipokuwa kwa uokoaji wa kitabibu ulioidhinishwa, watu walioambukizwa Ebola ya Bundibugyo au waliotambuliwa kama waliokaribiana na mgonjwa hawapaswi kuruhusiwa kusafiri kimataifa.
- Kudumisha mawasiliano ya wazi na abiria — Mashirika ya ndege yanapaswa kuwahakikishia wasafiri kwa kueleza wazi hatari ndogo ya maambukizi na hatua zilizopo za kulinda afya.
ICAO imesisitiza kuwa hatua hizi ni muhimu si tu kwa kulinda abiria na wafanyakazi wa anga bali pia kwa kudumisha imani ya umma na kuhakikisha usafiri wa anga unaendelea kwa ajili ya mahitaji ya kibinadamu na kiuchumi.
Nini Kamati ya Dharura ya WHO ilitangaza?
Kamati ya Dharura ya WHO ilikutana tarehe 19 Mei 2026, kufuatia uamuzi wa Mkurugenzi Mkuu kutangaza mlipuko huo kuwa PHEIC siku mbili kabla. Kamati ilikubaliana kwamba mlipuko wa sasa si janga la afya duniani.
