Wanawake Kivu Kaskazini waahidi kulinda amani na kupambana na habari potofu: MONUSCOWanawake Kivu Kaskazini waahidi kulinda amani na kupambana na habari potofu: MONUSCO

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, warsha hiyo imeandaliwa na kitengo cha masuala ya kiraia cha MONUSCO kwa ushirikiano na ofisi ya utafiti na usaidizi wa uhusiano wa Kimataifa nchini DRC (BEARIC) pamoja na mamlaka za jimbo hilo.

Washiriki wa fursa hiyo ni wanawake kutoka mashirika ya kijamii, asasi za kiraia, wanawake waliokimbia vita, walemavu, wajumbe wa vyama vya siasa, taasisi za kidini, na makundi ya vijana ambao kwa pamoja wamefundishwa kuhusu michakato ya amani inayoendelea nchini DRC, hasa ile inayofanyika maeneo mbalimbali duniani ikiwemo katika miji ya Washington( Marekani), Doha (Qatar), Luanda (Angola), na Nairobi (Kenya), huku wakihimizwa kufuata maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1325 na 2773 yanayohusu ushiriki wa wanawake kwenye amani na ulinzi wa raia.

Wito kwa wanawake kuchukua hatua madhubuti

Kutokana na hali ya usalama kuendelea kuwa tete mashariki mwa DRC, Afisa programu wa BEARIC na mwezeshaji wa warsha hiyo, Jean-Paul Lusenge, amefafanua lengo kuu akionesha umuhimu wa wanawake kutumia mbinu za utatuzi wa migogoro ili kuzuia vijana kujiunga na makundi ya waasi. 

“Tulitaka kuinua ari ya wanawake kuhusu changamoto zilizopo hivi sasa, hasa makubaliano ya Washington na Doha, na tusiwafanye kuwa watazamaji tu bali washiriki hai, kwa sababu nafasi yao ipo kwenye meza ya maamuzi” Amesema Lusenge

Ameeleza pia yale waliyotekeleza mpaka sasa “ Tumefanya kazi kwenye uongozi, utatuzi wa migogoro, na mbinu za utetezi, kwani nchi yetu inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji majibu ya namna mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utetezi na utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani. Ilikuwa muhimu kushirikisha maudhui ya makubaliano yanayoendelea sasa hivi ili kuzuia upotoshaji wa habari na ushawishi mbaya unaoweza kuwasukuma baadhi ya vijana kujiunga na makundi ya waasi”.

Wanawake waahidi kuchukua hatua katika ngazi ya jamii

Kwa upande wake, mshiriki Julienne Masika amesisitiza wanawake wamepewa nguvu ya kisheria kushiriki kwenye mazungumzo ya amani kuanzia ngazi ya kijiji hadi kikanda.

“Wanawake lazima washiriki katika kuzuia migogoro, hasa kuhusu ukatili unaotokana na migogoro hiyo. Sio tu ukatili wa kijinsia, kwa sababu kuna namna nyingi za ukatili. Kwa hiyo, wanawake lazima washirikishwe; lazima waweze kushawishi na kubadili maamuzi, kwa kuzingatia kwamba Azimio namba 1325 linatupa nguvu ya kushiriki katika mazungumzo ya amani katika ngazi zote ndani ya mfumo wa kuzuia, iwe ni katika ngazi ya ndani hapa Beni au katika ngazi ya kikanda,” amebainisha Julienne.

Makamu wa Rais wa Asasi ya Kiraia ya Kyambogho katika eneo la Lubero, Guilaine Kavira Mwangaza, ameeleza utayari wao wa kwenda kufanya kazi mashinani, “Tumejitolea kuelimisha na kuhamasisha wanawake wote ili kuchangia katika ushirikiano wa kijamii na kupambana na upotoshaji wa habari. Mafunzo haya yametuwezesha kuelewa vizuri masuala kadhaa na kurekebisha mitazamo fulani potofu. Kuhusu Azimio namba 1325, tutawahimiza wanawake kujisogeza mbele zaidi katika utekelezaji wake madhubuti. Na kuhusu mbinu za utetezi, sasa hivi tumewezeshwa vizuri zaidi kujua nini cha kuandika na kwa nani tunapaswa kuelekeza changamoto zetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *