
Katika barua yake iliyoandikwa kwa Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa, Dkt. Tedros amesema mlipuko huo ni changamoto kubwa kwa sababu unatokana na virusi tofauti na aina ya Ebola Zaire ambayo zamani ilikuwa na chanjo na matibabu.
“Kwa sasa hakuna chanjo wala matibabu yaliyoidhinishwa dhidi ya Ebola Bundibugyo,” amesema Dkt. Tedros huku akisisitiza kuwa hatua za haraka za jamii zinaweza kusaidia kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo na kuokoa maisha.
Iituri yabeba zaidi ya asilimia 90 ya maambukizi
Kwa mujibu wa ujumbe huo, zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wa Ebola wameripotiwa katika jimbo la Ituri, huku wagonjwa wengine wakiripotiwa majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Dkt. Tedros amesema anaelewa uchovu na mateso yanayowakabili wananchi wa Ituri ambao tayari wanakabiliana na malaria, njaa, ukosefu wa usalama na changamoto za maisha ya kila siku.
Amekumbusha kuwa tayari aliwahi kushuhudia mlipuko mkubwa wa Ebola kati ya mwaka 2018 na 2020 alipofanya ziara mara 14 katika maeneo ya Beni, Butembo, Katwa na Goma wakati wa mlipuko uliopita.
Changamoto Kubwa: Vita, hofu na kutokuaminiana
Katika ujumbe wake, Dkt. Tedros ameeleza kuwa changamoto kubwa katika kudhibiti Ebola si ugonjwa pekee, bali pia hali ya usalama na kutokuaminiana kwa jamii.
Amesema baadhi ya wafanyakazi wa afya waliwahi kushambuliwa huku vituo vya afya vikilengwa wakati wa milipuko iliyopita, jambo lililosababisha kupotea kwa muda muhimu wa kuokoa maisha.
Aidha, mapigano na kuhama kwa wananchi kutoka maeneo yao vinaendelea kuathiri juhudi za kuwafikia wagonjwa na kuwalinda wahudumu wa afya.
Kutokana na hali hiyo, Dkt. Tedros ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano katika maeneo yaliyoathirika ili kuruhusu huduma za afya kuwafikia wananchi.
“Hakuna sababu inayostahili kuwahukumu watu wasio na hatia kufa kutokana na ugonjwa unaoweza kuzuiwa,” amesema.
Jamii zatakiwa kufanya nini?
Dkt. Tedros amesisitiza kuwa licha ya kukosekana kwa chanjo na tiba maalum, jamii zina nafasi kubwa ya kusaidia kudhibiti maambukizi kwa hatua za haraka.
Miongoni mwa hatua alizozitaja ni:
Kujitokeza mapema hospitalini
Amesihi wananchi wanaohisi dalili za Ebola au wanaowajua wagonjwa kutafuta matibabu mapema bila kusubiri hali kuwa mbaya.
Kwa mujibu wake, huduma za mapema zinaweza kuongeza nafasi ya kupona na kusaidia kuzuia maambukizi zaidi.
Kushirikiana na wahudumu wa afya
Dkt. Tedros amesema mafanikio ya kudhibiti mlipuko yanategemea ushirikiano kati ya jamii na wahudumu wa afya.
Ametoa wito kwa wananchi kuamini taarifa rasmi za afya na kuwasaidia wahudumu wanaofanya kazi katika mazingira magumu.
Vijana kuelimisha jamii
Katika ujumbe maalum kwa vijana wa Ituri, amewataka kutumia sauti zao kuelimisha marafiki, familia na jamii kuhusu Ebola.
“Hofu, uvumi na ukimya vinaweza kuruhusu virusi kuendelea kuenea.”
Mazishi salama na yenye heshima
WHO pia imehimiza jamii kufuata taratibu salama za mazishi ili kupunguza hatari ya maambukizi huku ikiheshimu tamaduni za familia zilizopoteza wapendwa wao.
WHO yaahidi kuendelea kushikamana na DRC
Dkt. Tedros amesema WHO inaendelea kufanya kazi chini ya uongozi wa Serikali ya DRC pamoja na washirika mbalimbali kuhakikisha mlipuko huo unadhibitiwa.
Aidha, ametangaza kuwa atawasili Bunia mji mkuu wa jimbo la Ituri kukutana na viongozi wa jamii na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi wa Ituri.
“Huu ni mlipuko wa 17 wa Ebola nchini DRC. Mmeweza kushinda milipuko yote iliyopita, na naamini mtashinda huu pia,” amesema.
Ametamatisha waraka wake huo wa lugha ya Kiswahili wenye maneno 1370 kwa kuwahakikishia wananchi wa Ituri kuwa hawajasahauliwa na kwamba dunia inaendelea kushuhudia ujasiri wao katika kukabiliana na mlipuko huo mpya wa Ebola.
