
Akizungumza mjini New York na UN News baada ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, Balozi Mavura amesema ujumbe aliompelekea Katibu Mkuu kutoka kwa Rais wa Tanzania ni wa kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika kipindi ambacho dunia inapitia changamoto kubwa za usalama na maendeleo.
“Tanzania tutaendelea kuwa upande wa Umoja wa Mataifa, upande wa ushirikiano wa kimataifa, kuhakikisha kwamba ajenda zake zinakamilika katika masuala ya ulinzi wa amani, maendeleo pamoja na haki za binadamu,” amesema.
Tanzania yajivunia mchango wa walinda amani
Katika mahojiano hayo, Balozi Mavura amesema moja ya maeneo ambayo Tanzania imeendelea kujipambanua ni katika operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa.
Amesema Tanzania kwa sasa ni miongoni mwa nchi kumi zinazoongoza kwa kuchangia wanajeshi wengi katika misheni za kulinda amani duniani, jambo ambalo amesema linaonesha dhamira ya nchi katika kuifanya dunia kuwa salama zaidi.
“Tumekuwa tukitumia majeshi yetu kwenye maeneo mbalimbali kwa ajili ya kulinda amani na tumekuwa tukifanya vizuri sana,” amesema.
Kwa mujibu wake, Tanzania inaona bado ipo nafasi ya kuongeza mchango wake zaidi, hasa wakati ambapo migogoro na changamoto za kiusalama zinaendelea kuongezeka duniani.
“Tunadhani tunaweza kutoa mchango wetu zaidi kwenye eneo hili,” ameongeza.
Safari kuelekea Baraza la Usalama
Balozi huyo pia alizungumzia azma ya Tanzania ya kuwania nafasi ya ujumbe usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa 2029-2030, akisema hatua hiyo italisaidia taifa kuongeza sauti yake katika juhudi za kurejesha amani duniani.
Amesema hata kama Tanzania si taifa lenye nguvu kubwa za kijeshi au kifedha kama baadhi ya mataifa makubwa, bado lina nguvu ya ushawishi kupitia diplomasia, maridhiano na sauti yake ya amani.
“Bado tuna nguvu ya sauti. Tunaweza kutumia sauti yetu vizuri,” amesema.
Ameeleza kuwa Tanzania imekuwa na historia ya kuwa mpatanishi na msuluhishi katika migogoro mbalimbali, na sasa inalenga kutumia uzoefu huo kuimarisha mshikamano wa kimataifa.
“Tunataka kutumia fursa hiyo kuona namna gani tunaweza kutoa mchango kuifanya dunia kuwa sehemu salama ya kuishi kwa watu wote.”
Mageuzi ya Umoja wa Mataifa yasikate maendeleo
Katika kipindi hiki ambapo Umoja wa Mataifa unakabiliwa na changamoto za kifedha na mjadala wa mageuzi ya mfumo wake ukiendelea, Balozi Mavura amesema Tanzania inaunga mkono mageuzi yatakayoongeza ufanisi, lakini bila kuathiri programu za maendeleo kwa nchi zinazoendelea.
Amesema mataifa kama Tanzania bado yanahitaji mchango mkubwa wa Umoja wa Mataifa katika maendeleo, hivyo kupungua kwa fedha hakupaswi kuwa sababu ya kupunguza huduma muhimu kwa wananchi.
“Tunataka kuhakikisha kwamba kupungua kwa fedha kisiwe kisingizio cha kukata programu za maendeleo,” amesema.
Amesisitiza umuhimu wa kutafuta uwiano kati ya mageuzi na ufanisi kwa upande mmoja, na kuendelea kusaidia nchi zinazohitaji zaidi msaada wa Umoja wa Mataifa kwa upande mwingine.
Ahadi kwa Watanzania
Akihitimisha mahojiano hayo, Balozi Mavura amewahakikishia Watanzania kwamba ataitumikia nchi kwa weledi, maarifa na kujituma kikamilifu katika jukwaa la Umoja wa Mataifa.
“Watanzania wategemee kama nilivyoapa mbele ya Mheshimiwa Rais, nitawatumikia kwa uwezo wangu wote, weledi wangu wote na maarifa yangu yote kuhakikisha kwamba maslahi yao na maslahi ya nchi yetu yanazingatiwa katika eneo hili ambapo maslahi ya dunia yanatengenezwa.”
