
Dar es Salaam. Kama wewe unaamini usemi kuwa mdaiwa huwa hafungwi, basi unajidanganya na hii ni baada ya Mahakama Kuu, kumpa siku 21 mfanyabiashara wa jijini Dar es Salaam kulipa Sh50 milioni au akabiliwe na kifungo cha miezi sita kama mfungwa wa kiraia.
Sasa kama atashindwa kulipa ndani ya muda huo, Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, imetoa amri mfanyabiashara huyo akamatwe na kupelekwa gerezani kwa miezi sita na mdai atalipa Sh300,000 kila mwezi za matunzo yake.
Uamuzi huo umetolewa na Jaji Elizabeth Mkwizu wakati anatoa uamuzi wake kutokana na maombi namba 490 ya 2026 yaliyofunguliwa na Dorosella Bishanga dhidi ya Kidzone Pre-School and Adventures Center Ltd na Princess Basikiti.
Katika maombi yake, Bishanga aliiomba Mahakama itoe amri ya kukamatwa na kuwekwa kizuizini gerezani kama Basikiti (mfungwa wa kiraia) baada ya Bishanga kukazia hukumu na kushindwa kupata mali za mdaiwa huyo.
Mwaka 2024, Bishanga alifungua kesi ya madai namba 490, akiomba shule inayomilikiwa na mdaiwa huyo na wadaiwa wengine wawili, Tafadzwa Mutizwa na Mick Thomas, wamrejeshee Sh40.5 milioni.
Fedha hizo alikuwa ameziwekeza katika Shule ya Kidzone kwa makubaliano ya kununua hisa lakini wajibu maombi wakawa hawampi faida wala taarifa ya fedha ya biashara hiyo ya shule lakini hawakumshirikisha katika usimamizi wa biashara.
Katika kesi hiyo, wadaiwa hao wanne walikiri kupokea fedha hizo za uwekezaji kutoka kwa Bishanga, lakini wakashilia msimamo kuwa biashara hiyo ilikuwa inajiendesha kwa hasara, hivyo wakaamua kusitisha shughuli zake mwaka 2022.
Baada ya kusikiliza pande zote, Mahakama iliona mdai ambaye ni Bishanga alikuwa ameshindwa kuthibitisha kiasi cha faida iliyopatikana, lakini akaweza kuthibitisha uwekezaji wake na wadaiwa wakashindwa kuthibitisha hasara waliyodai.
Mahakama ikawaamuru wadaiwa namba moja na mbili ambao ni Shule ya Kidzone na Princes Basikiti, kumrejeshea Bishanga Sh40.5 milioni, kulipa fidia ya uharibifu wa jumla Sh10 milioni, kulipa riba ya asilimia 7 kwa mwaka na gharama za kesi.
Wadaiwa namba tatu na nne ambao ni Tafadzwa Mutizwa na Thomas hawakutokea mahakamani licha ya kupelekewa wito hivyo ikasikilizwa bila wao kuwapo hasa kwa kuwa amri ambayo ingetolewa, ilikuwa haiwagusi moja kwa moja.
Mabishano ya kisheria
Wakati maombi ya amri ya kumkamata Basikiti na kumtupa gerezani kama mfungwa wa kiraia yaliposikilizwa Mei 19, 2026, muombaji aliwakilishwa na wakili Joseph Rugambwa na wajibu maombi wakawakilishwa na wakili Pachal Kihamba.
Akiwasilisha hoja za kuunga mkono maombi hayo, wakili Rugambwa alisema wamewasilisha maombi ya kukamatwa kwa Basikiti kwa kuwa jitihada za kutekeleza hukumu ya Mahakama kwa kukamata mali zake imeshindikana.
Wakili huyo alieleza baada ya kutolewa kwa hukumu ya kesi ya madai ya mwaka 2024, mteja wake alifanya jitihada za kubaini mali za mdaiwa lakini hakufanikiwa ndipo aliporudi mahakamani ikaelekeza afunguo maombi ya kumkamata.
Kwa mujibu wa wakili huyo, baada ya kushindwa kubaini mali za mdaiwa huyo, hakuna njia nyingine ya kutekeleza hukumu ya Mahakama iliyopo zaidi ya maombi ya kumkamata na kumweka kizuini gerezani kama mfungwa raia.
Hata hivyo, wakili wa wajibu maombi alipinga maombi hayo akisema moja ya vigezo muhimu vya kuzingatiwa ni uthibitisho kwamba mdaiwa alitenda kwa nia au nia mbaya ya kumnyima haki mdaiwa mwenye ya kufurahia matunda ya amri.
Wakili huyo alidai kuwa madai ya mwombaji kuwa juhudi zimefanywa kufuatilia mali ya mdaiwa ilikuwa tu ni madai matupu bila kuungwa mkono na ushahidi.
Alidai kuwa mwenye amri au tuzo ya Mahakama alihitajika kuthibitisha kwa hakika juhudi zinazodaiwa za kufuatilia mali na kushindwa badala ya kutoa tu madai katika hati ya kiapo na kwamba mdai alitakiwa amalize njia zote zilizopo kudai.
Uamuzi wa Mahakama
Katika uamuzi wake alioutoa Mei 29, 2026 na nakala ya uamuzi huo kuwekwa katika tovuti ya Mahakama Mei 30,2026, Jaji Mkwizu alisema kumkamata mdaiwa na kumweka gerezani ni hatua ya mwisho baada ya kujiridhisha kuwa mdaiwa hataki kulipa deni au anapuuza kutekeleza amri hiyo ya Mahakama.
Katika shauri hilo, Jaji alisema hakuna ubishi kuwa kuna tuzo ya Mahakama ambayo mleta maombi alikuwa ameshinda kortini mwaka 2024 na kwamba tuzo hiyo aliyoipata baada ya kushinda kesi, haijatimizwa hadi kufikia anatoa uamuzi.
“Katika kesi hii, mwombaji anasema alifanya juhudi kufuatilia mali zinazoweza kuhamishika na zisizohamishika, zinazomilikiwa na wadaiwa lakini ameshindwa kupata mali yoyote kama hiyo,”alisema jaji.
“Yeye aliongeza kusema kuwa biashara pekee inayoweza kutambulika iliyohusishwa na wajibu maombi ni Kidzone Day Care Centre ambayo wamekoma kufanya shughuli na hana njia nyingine yoyote ya kumpatia kipato.
“Ingawa wajibu maombi walipinga tuhuma hizo, hawakufanya hivyo kufichua katika hati yao ya kiapo cha kukanusha, mali yoyote iliyopo inayoweza kuambatishwa kama mali ya kampuni au Mdaiwa wa Pili.
“Kwa maoni yangu, mara mwombaji anapoapa kwamba alitafuta mali za wadaiwa bila kufanikiwa, mzigo wa ushahidi unahamishiwa kwa wajibu maombi ambao wako katika nafasi nzuri ya kujua na kufichua uwepo wa mali zao wenyewe.
“Wajibu maombi hawawezi tu kukana madai hayo huku wakihodhi taarifa ambazo zimo ndani ya ufahamu wa.”
“Baada ya kuzingatia ushahidi ulio mbele yangu kwa jumla wake, nimeridhika kwamba mwombaji ameweka misingi ya kutosha ya utoaji wa amri ya kukamatwa na kuwekwa kizuizini gerezani kwa mjibu maombi wa pili (Basikiti),”alisema.
“Ninaamuru kuwa kiasi kinachodaiwa kisipolipwa kikamilifu ndani ya siku 21 kuanzia tarehe ya hukumu hii, basi mjibu maombi wa pili atakamatwa na kufungwa kama mfungwa wa kiraia kwa muda wa miezi sita.
“Mwombaji atawajibika kulipa fedha za kujikimu na gharama za matunzo ya mdaiwa ambayo ni Sh300,000 kwa kila mwezi. Kiasi kilichotajwa kitalipwa mapema mwanzoni mwa kila mwezi,”alisisitiza Jaji Mkwizu.
Jaji Mkwizu alisema malipo ya awamu ya kwanza yatalipwa kwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam baada ya kukamatwa kwa mdaiwa na awamu zinazofuata zitatumwa kwa ofisa mfawidhi wa gereza.
Jaji alisema endapo mdai atashindwa kuzingatia wajibu wa kulipa posho ya kujikimu kama ilivyoainishwa na sheria, basi mdaiwa ataachiliwa mara moja kutoka kwa kizuizi cha raia katika gereza atakalokuwa anashikiliwa.