MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori ‘General’, amefafanua nafasi ya mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed Dewji (MO), akisisitiza bilionea huyo hawezi kuondoka klabuni hapo kwa uamuzi binafsi kwa kuwa yupo kwa mujibu wa mkataba wa uwekezaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Magori amesema tofauti na mtazamo wa baadhi ya mashabiki, MO si mfadhili wa Simba bali ni mwekezaji kupitia kampuni ya MO Dewji Company Limited, inayomiliki asilimia 49 ya hisa za Simba Sports Club Limited iliyosajiliwa BRELA.
“MO hawezi kuiacha Simba kwa sababu yupo kimkataba. Hawezi kuamka tu na kusema anaondoka na kuiacha Simba. Hilo suala halipo. Ukiangalia nyaraka za uwekezaji utaona wazi, wala si jambo la siri,” amesema Magori.
Aliongeza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakichanganya kati ya mfadhili na mwekezaji, hali inayosababisha tafsiri zisizo sahihi kuhusu nafasi ya MO ndani ya klabu hiyo.
“Mfadhili anaweza kuamua kuondoka wakati wowote, lakini MO ni sehemu ya Simba. Nilisikia wengine wakisema wanampa saa kadhaa aondoke, jambo ambalo linaonyesha hawafahamu uhalisia wa suala hili,” amesema.
ANATOA BILIONI 4-5 KILA MSIMU
Magori pia alifichua kuwa MO amekuwa akitoa kati ya Sh 4 bilioni hadi 5 kila msimu kwa ajili ya usajili, fedha ambazo amesema ni za hiari na zipo nje ya makubaliano ya uwekezaji.
“MO anatoa kati ya Sh 4 bilioni hadi 5 kila msimu kwa ajili ya usajili kwa hiari yake mwenyewe, nje ya mkataba wa uwekezaji. Lengo lake ni kuona Simba inakuwa klabu kubwa Afrika,” amesema.
Alihoji madai ya mara kwa mara kwamba MO hatoi fedha klabuni, akieleza kuwa mahitaji makubwa ya usajili na uendeshaji wa timu yanahitaji fedha nyingi ambazo zimekuwa zikipatikana kupitia mchango wake.
“Tunapozungumzia kusajili straika na viungo wa kiwango cha juu, unakuta mahitaji yanafika Sh 4 bilioni. Mbali na hilo, kuna gharama za kila mwezi za mishahara, safari na uendeshaji wa timu sisi hatuna hela, yeye anatoa kutusaidia,” amesema.
BILIONI 20 ZA UWEKEZAJI ZIPO
Kuhusu mjadala wa fedha za uwekezaji za Sh 20 bilioni, Magori amesema kiasi hicho tayari kiliwasilishwa na MO na kimehifadhiwa katika akaunti maalumu ya Escrow.
“Fedha za uwekezaji za Sh 20 bilioni zipo. Ziliwekwa kwenye akaunti ya Escrow katika Benki ya Equity na zitahamishiwa Simba mara baada ya mchakato wa mabadiliko kukamilika rasmi, kila mtu anatakiwa kuelewa hili kwa hiyo wale ambao wanaamini hajatoa hela ndiyo wachukue hili sasa,” amesema.
KUHUSU MADAI YA KUIDAI SIMBA
Magori pia alipinga taarifa zilizowahi kusambaa zikidai kuwa MO ameandika barua ya kuidai Simba fedha alizotumia ndani ya klabu hiyo.
Amesema kilichopo ni ombi la mwekezaji huyo kutaka kupata taarifa kamili za gharama alizozitumia tangu aanze kuwekeza ndani ya Simba.
“Si kweli kwamba alikuwa anaidai Simba. Alichoandika ni kutaka kujua ametumia kiasi gani tangu aanze kuwekeza. Hata kama angesema anadai, Simba ingewezaje kumrudishia fedha hizo?” alihoji.
Aliongeza kuwa wadau wa soka wanapaswa kuwaheshimu watu wanaotoa fedha zao kwa ajili ya maendeleo ya klabu.
“Tunahitaji kuwaheshimu hawa wanaowekeza na kutoa fedha zao kwa mapenzi ya kuisaidia klabu kupata mafanikio,” amesema Magori.