Katika ujumbe wake kwa Mkutano wa Tisa wa Kila Baada ya Miaka Miwili wa Nchi Wanachama kuhusu Mpango wa Utekelezaji wa Kudhibiti Silaha Ndogo na Nyepesi uliofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani Katibu Mkuu amesema mazingira ya usalama duniani yamebadilika kwa kiasi kikubwa tangu kupitishwa kwa Mpango huo miaka 25 iliyopita.

“Migogoro inayotumia silaha inaongezeka. Migawanyiko inaendelea kuongezeka. Matumizi ya kijeshi yanapanda kwa kasi,” amesema, akitaja changamoto mpya zinazojitokeza kama vile silaha zinazotengenezwa kwa teknolojia ya uchapishaji wa 3D na silaha zisizoweza kufuatiliwa maarufu kama ghost guns ambazo zinazidi kusambaa katika masoko haramu.

Katibu Mkuu amebainisha kuwa uhamishaji wa silaha kutoka katika mifumo halali kwenda kwenye mikondo haramu bado ndiyo njia kuu inayowezesha makundi yenye silaha kupata silaha zinazochochea vurugu na ukosefu wa usalama.

Amesema silaha hizo zinachangia ugaidi, uhalifu wa kupangwa na ukatili wa kijinsia, huku pia zikihatarisha maisha ya walinda amani na kuzuia upatikanaji wa misaada ya kibinadamu kwa watu wanaohitaji.

Akinukuu takwimu za Shirika la Kimataifa la Polisi (INTERPOL), Guterres amesema kuna zaidi ya rekodi milioni mbili za silaha zilizopotea, kuibwa au kusafirishwa kinyume cha sheria ambazo bado zipo katika mzunguko duniani.

Amezitaka nchi wanachama kutumia Mpango wa Utekelezaji kama msingi wa kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kupitia kubadilishana taarifa za kiintelijensia, msaada wa kiufundi na kujenga uwezo.

Katibu Mkuu pia amehimiza nchi kubuni suluhisho mpya za kukabiliana na changamoto zinazoletwa na teknolojia mpya pamoja na kuzuia uhamishaji haramu wa silaha, huku zikidhibiti mtiririko wa silaha haramu na kuziba mianya ya kisheria inayowezesha biashara hiyo.

“Ni lazima tuhakikishe kuwa Mpango wa Utekelezaji unakidhi changamoto za leo,” amesema.

Guterres amewahimiza wajumbe wanaokutana New York kupitisha hati ya makubaliano itakayosaidia kulinda jamii dhidi ya tishio la silaha ndogo na nyepesi haramu.

“Kwa pamoja, tujenge jamii salama zaidi na dunia yenye usalama mkubwa zaidi,” amehitimisha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *