
Idadi ya visa vilivyothibitishwa vya ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) imevuka 300 kufikia Jumatatu.
Hayo ni kwa mujibu wa takwimu za karibuni zilizotolewa na Wizara ya Afya ambapo idadi ya vifo vinavyohusishwa na virusi hivyo imeongezeka na kufikia 48.
Wizara hiyo imesema mlipuko huo unaendelea kuenea na sasa umeathiri maeneo 23 ya huduma za afya katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Katika jimbo la Ituri, ambalo limekumbwa na miaka mingi ya ukosefu wa usalama, visa vilivyothibitishwa vimezidi 260.
Mamlaka za afya zilisema upinzani kutoka kwa jamii katika mji mkuu wa jimbo, Bunia, na mji wa kaskazini mashariki wa Nizi, pamoja na uvumi na taarifa potofu, vinafanya juhudi za kudhibiti mlipuko huo kuwa ngumu zaidi.
Maafisa walisema Jumatatu kuwa wagonjwa wanne wamepona na kuruhusiwa kutoka Kituo cha Tiba cha Kiinjili mjini Bunia.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus, alihitimisha ziara yake nchini Kongo siku ya Jumatatu baada ya kukutana na Rais Felix Tshisekedi kujadili hatua za kukabiliana na mlipuko wa Ebola wa aina ya Bundibugyo.
Kwingineko, Mamia ya vijana katika mji wa Nanyuki nchini Kenya wameandamna kupinga hatua ya serikali ya kuruhusu kujengwa kituo cha kupokea wagonjwa wa Ebola raia wa Marekani, katika kambi ya jeshi ya Laikipia.
Maandamano yamejiri siku chache baada ya mahakama kuu ya Kenya kutoa agizo la kusitishwa ujenzi wa kituo hicho pamoja na kuzuiwa kuingia raia wa kigeni walioambukizwa virusi hivyo, hadi itakaposikilizwa kesi iliyowasilishwa na chama cha wanasheria nchini Kenya na taasisi inayosimamia katiba.