Walinzi wengine wawili wa amani walijeruhiwa katika shambulio hilo na wanaendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha afya cha UNIFIL kusini mwa nchi hiyo.

“Katibu Mkuu analaani kuuawa kwa Sajenti Milovan Jovanović,” amesema Msemaji wa Katibu Mkuu, Stéphane Dujarric, katika taarifa iliyotolewa leo mjini New York Marekani akiongeza kuwa uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Rambirambi na wito wa uwajibikaji

Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia, marafiki na wafanyakazi wenzake na marehemu pamoja na Serikali na wananchi wa Jamhuri ya Serbia.

Pia amewatakia ahueni ya haraka walinzi wa amani waliojeruhiwa. Akisisitiza uzito wa tukio hilo, amesema kuwa, “Mashambulizi dhidi ya walinzi wa amani lazima yakome,” akionya kuwa vitendo hivyo ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na vinaweza kuchukuliwa kama uhalifu wa kivita.

Idadi ya vifo vya walinda amani yaongezeka

Tukio hilo limefikisha idadi ya walinda amani wa UNIFIL waliouawa kufikia saba tangu kuongezeka kwa mapigano tarehe 2 Machi 2026, huku wengine kadhaa wakijeruhiwa.

Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande zote zinazohusika kuheshimu wajibu wao chini ya sheria za kimataifa na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa.

“Mashambulizi yote dhidi ya walinzi wa amani lazima yachunguzwe haraka, na wahusika wafikishwe mbele ya sheria na kuwajibishwa ipasavyo,” amesisitiza.

Wito mpya wa kuheshimu sitisho la mapigano

Katibu Mkuu pia ametoa wito mpya kwa pande zote kuheshimu sitisho la mapigano lililotangazwa tarehe 16 Aprili 2026 na kusisitiza dhamira ya Umoja wa Mataifa ya kuunga mkono juhudi za kidiplomasia za kuongeza muda wa sitisho hilo pamoja na utekelezaji kamili wa Azimio Namba 1701 la Baraza la Usalama. Aidha, ametoa pongezi kwa wanawake na wanaume wote wanaohudumu katika mpango wa UNIFIL, akisisitiza “umuhimu wa usalama wao na uhuru wa UNIFIL kutekeleza majukumu yake ya kulinda amani nchini Lebanon.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *