
Taarifa ya IOM iliyotolewa leo Juni 05 mjini Port-au-Prince, Haiti na Geneva, Uswisi zaidi ya nusu ya waliokimbia ni wanawake na wasichana, hali inayoonesha kuzorota kwa suluhu ya janga la kibinadamu linaoathiri maeneo ya mijini na vijijini.
IOM imesema janga hilo katika hatua ya kutisha zaidi huku ghasia zikienea hadi maeneo yaliyokuwa yakichukuliwa kuwa salama. Mwezi Mei pekee, zaidi ya watu 18,000 walikimbia makazi yao kufuatia vurugu mpya katika eneo la Cité Soleil, na kufanya idadi ya wakimbizi wa ndani katika mji mkuu, Port-au-Prince, kuzidi 300,000 kwa mara ya kwanza.
Katika wiki za hivi karibuni, mashambulizi ya makundi yenye silaha katika Eneo la Kusini-Mashariki ya Haiti pia yamesababisha zaidi ya watu 5,000 kuhama. Hali hiyo inaonesha kuwa hata maeneo yaliyokuwa yakitumika kama hifadhi kwa waliokimbia vurugu sasa yanageuka kuwa maeneo mapya ya migogoro na uhamaji wa watu.
Sababu zaidi
Janga hilo linachangiwa zaidi na kurejeshwa kwa nguvu kwa zaidi ya Wahaiti 110,000 kutoka mataifa mengine tangu mwanzo wa mwaka huu 2026. Wengi wao hurejea bila rasilimali za kujikimu na hukuta jamii ambazo tayari zinakabiliwa na uhaba wa huduma muhimu, huku watoto, wanawake wajawazito na makundi mengine yaliyo hatarini wakibeba mzigo mkubwa zaidi.
IOM imetahadharisha kuwa uhaba wa makazi, chakula, maji safi, huduma za afya na msaada wa kisaikolojia unaendelea kuongezeka, hasa wakati msimu wa vimbunga wa Atlantiki ukiwa umeanza. Shirika hilo linaendelea kutoa msaada wa dharura lakini linasisitiza umuhimu wa uwekezaji endelevu katika misaada ya kibinadamu na juhudi za kujenga uwezo wa jamii ili kusaidia Wahaiti kurejesha maisha yao.