ARUSHA: KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi amewataka wananchi kusimama kidete katika kukemea vitendo vya ukatili dhidi ya watoto pamoja na mmomonyoko wa maadili.

Lengo ni kulinda ustawi wa familia na kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama yanayowawezesha kutimiza ndoto zao.

Kihongosi ametoa mwito huo leo Juni 5,2026 alipotembelea na kushiriki kikao katika Shina Namba Saba Kata ya Moivo wilayani Arumeru mkoani Arusha, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika Kanda ya Kaskazini.

Mwito huo umefuatia hoja wananchi wa shina hilo walizoziwasilishwa kama changamoto zinazowakabili katika eneo hilo likiwemo suala la ubakaji na ulawiti wa watoto na matendo ya uhalifu yakihusisha matumizi ya dawa za kulevya.

Akijibu hoja hizo Kihongosi amemtaka kila mzazi kuwa mlinzi wa watoto wake na wa wenzake, akisisitiza ushirikiano kati ya wamanchi, serikali na chama kukemea tabia zisizofaa bila kuona haya wala aibu wala kuwalinda wahalifu.

“CCM tunayakemea kwa nguvu zote matendo haya kwani hayakubaliki, kwa sababu unapokwenda kumbaka au kumlawiti mtoto mdogo moja inamuathiri kisaikolojia pili ina muharibia malengo ambayo alikuwa nayo, pia inapeleka simanzi ndani ya familia kitu ambacho si kizuri,” amesema Kihongosi

Kihongosi amewataka wazazi na walezi kuacha kumaliza mambo kifamilia, kwa kupokea fedha au Ng’ombe inapotokea mtoto ameathirika na matukio ya ubakaji na ulawiti ili kulinda ustawi wa watoto hao na jamii kwa ujumla.

Amesema kumaliza mambo kifamilia kesi inaharibika wanafifisha juhudi za serikali katika kupambana na haya mambo, na kusababisha haki ishindwe kutendeka.

Amewasisitiza kuacha kunyoosha vidole kwa serikali pekee yake badala yake wungane kwa dhamira ya dhati kwamba hilo jamno limetosha na kuacha tamaa ya kupokea vitu vidogo ili kulinda ustawi wa watoto wao.

Awali, hoja hizo ziliwasilishwa na wananchi wawili ya kwanza iliwasilishwa na Agness Lembris ambaye alilalamikia kuhusu mmomonyoko wa maadili unaohusisha matumizi ya dawa za kulevya uliokithiri katika eneo hilo la Moivo.

Agness amedai wanaomba serikali iwasaidie kutafuta mwarobaini matumizi ya dawa za kulevya, kwani suala hilo limekuwa sugu katika Kata ya Moivo kwani hata wahalifu wakikamatwa wanaachiwa na kuendelea na tabia hiyo.

Pia changamoto ya pili kuhusu suala la ubakaji na ulawiti wa watoto iliwasilishwa na mwananchi Vicky Alex akidai kuwa matukio hayo yamekuwa yakikithiri hali inayohatarisha ustawi wa watoto wao katika eneo hilo

“Tunaomba serikali kuwadhibiti hawa waarifu kwani watoto wanaobakwa ni chini ya umri wa miaka 18 hali inayowapelekea kupoteza ndoto zao,” amesema Vicky.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *