Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu amesema miaka 11 iliyopita imekuwa ndiyo yenye joto zaidi kuwahi kurekodiwa katika historia ya binadamu.

“Na katika Siku hii ya Mazingira Duniani, ishara za tahadhari zipo kila mahali.”

Ameongeza kuwa madhara ya uharibifu wa mazingira sasa yanaonekana wazi kupitia hewa iliyochafuliwa, ardhi iliyoharibiwa, mifumo ya ikolojia inayoporomoka na kupotea kwa bioanuwai.

Athari zatishia afya na uhakika wa chakula

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira si tatizo la baadaye bali ni janga linaloathiri maisha ya watu hivi sasa.

“Kudhuru afya, kuharibu makazi na kuongeza baa la njaa,” amesisitiza, akielezea athari zinazowakumba mamilioni ya watu duniani, hasa wale walio katika mazingira magumu zaidi.

Ameonya kuwa dunia iko kwenye njia ya kuvuka kiwango cha nyuzi joto 1.5, hatua ambayo inaweza kusababisha madhara makubwa zaidi kwa binadamu na mazingira.

“Kila kiwango kidogo cha nyuzi joto kinaleta madhara makubwa hasa kwa wale walio hatarini zaidi,” amesema.

© Unsplash/Anne Nygård Gesi hatari za methane zinachangia mabadiliko ya hali ya hewa.

Uzalishaji wa hewa chafu lazima usite

Guterres ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na za dhati ili kupunguza kasi ya ongezeko la joto duniani.

“Jukumu letu ni kuhakikisha ongezeko hilo ni dogo, kwa muda mfupi na salama iwezekanavyo na kurejesha chini haraka viwango vya joto,” amesema.

Amesisitiza kuwa hatua hiyo inahitaji kupunguza kwa kasi uzalishaji wa gesi chafuzi zinazochangia mabadiliko ya tabianchi.

Nishati mbadala ndio suluhu endelevu

Katika ujumbe huo Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa kuharakisha mpito kutoka matumizi ya mafuta ya kisukuku kwenda kwenye nishati mbadala.

“Kuharakisha mpito wa haki kutoka mafuta ya kisukuku kwenda nishati mbadala ni njia pekee endelevu ya kupunguza gharama na kufikia usalama wa kweli wa nishati,” amesema.

Pia ametaja kupunguza uzalishaji wa gesi ya methani kama moja ya hatua za haraka na nafuu zaidi za kupunguza ongezeko la joto katika miaka ya karibu.

© UNDP Mradi pia umesaidia kurejesha maeneo ya misitu yaliyoharibiwa kupitia mbinu za upandaji miti kavu huko Chakwal, Punjab.

Misitu, ardhi na bahari vilindwe

Amehimiza mataifa kuongeza juhudi za kulinda misitu, ardhi na bahari, huku yakiziwezesha jamii zinazokabiliwa na madhara ya tabianchi kujenga uwezo wa kukabiliana nayo.

Aidha, amezitaka nchi zilizoendelea kutimiza ahadi zao za ufadhili wa masuala ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea.

“Kutimiza ahadi za ufadhili wa fedha kwa ajili ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea ni kuokoa maisha, kulinda njia za kujipatia riziki na kuimarisha uchumi,” mesema.

“Huu Ndio Wakati wa Kuchukua Hatua”

Akihitimisha ujumbe wake, Katibu Mkuu ametoa wito wa hatua za haraka kabla hali haijawa mbaya zaidi.

“Huu ndio wakati wa kuchukua hatua kwa ajili ya mazingira yetu na mustakabali wetu.”

Kauli hiyo inakuja wakati dunia ikiendelea kushuhudia matukio makubwa ya hali mbaya ya hewa, ukame, mafuriko na kupungua kwa bioanuwai, mambo yanayochochewa na mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *