Walijiunga na mtetezi mashuhuri wa bahari Sylvia Earle na mvumbuzi Fabien Cousteau kuadhimisha uzinduzi ripoti ya Tathmini ya Bahari ya Dunia, (WOA), ripoti pana iliyofafanuliwa katika hafla hiyo kama “huenda ikawa nyaraka muhimu zaidi kuwahi kuandikwa kuhusu bahari.”

Ripoti hiyo, inayotarajiwa kuzinduliwa katika Siku ya Bahari Duniani tarehe 8 Juni, ina kurasa 1,600 na ni matokeo ya zaidi ya miaka mitano ya kazi iliyofanywa na wataalamu 550 kutoka nchi 86. Inatoa muhtasari wa kina wa shinikizo zinazoongezeka dhidi ya bahari pamoja na hatua zinazohitajika ili kuilinda.

Akizungumza katika hafla hiyo, Steven Hill, Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Sheria, amesema tathmini hiyo “inaimarisha ujumbe ulio wazi kabisa: sayansi ni ya lazima.”

Amesema ripoti hiyo inatoa msingi wa “kuelewa mabadiliko makubwa yanayoendelea kutokea, kuanzia yale yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi hadi upotevu wa bioanuwai, na pia kuandaa hatua madhubuti katika ngazi za mitaa na kimataifa.”

© Ujumbe wa Kudumu wa Uholanzi Steven Hill, Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Sheria akizungumza katika utangulizi wa uzinduzi wa Tathmini ya Tatu ya Hali ya Bahari duniani uliofanyika kwenye Klabu ya Wavumbuzi jijini New York, Marekani Juni 4, 2026

Mambo ambayo bado hatuyajui

Licha ya miongo kadhaa ya maendeleo, maeneo makubwa ya bahari, hasa bahari kuu za kina kirefu, bado hayajaeleweka vizuri.

Sylvia Earle, mwanasayansi mkongwe na maarufu wa masuala ya bahari, ameonya kwamba ripoti hiyo pia inaonesha ukubwa wa kazi ambayo bado inahitajika kufanywa.

“Jambo moja ambalo pia lazima lifanywe, na ambalo litahitaji maandiko mengi zaidi, ni kuelewa kwa kina ukubwa wa yale ambayo bado hatuyajui,” amesema.

Akinukuu kwa namna inayofanana na kauli maarufu ya Mark Twain kwamba, “Kinachotuingiza matatizoni si kile tusichokijua, bali ni kile tunachodhani tunakijua kwa uhakika ilhali si kweli,” Bi. Earle amesema kwamba wanasayansi wa sasa wanajua mengi zaidi kuliko vizazi vilivyotangulia, lakini lazima waendelee kutambua kwamba bado kuna mengi yasiyojulikana.

“Hatupaswi kuwa na matarajio makubwa sana kwamba tayari tuna majibu yote sahihi,” ameongeza.

Maarifa pekee hayatoshi

“Maarifa pekee hayatoshi,” amesema Bwana Hill. “Tuko katika kipindi ambapo mifumo ya ikolojia ya bahari inakaribia viwango hatari vya mabadiliko, na ambapo maamuzi tunayofanya, yanayotegemea sayansi bora inayopatikana, yataamua mustakabali wa bahari na manufaa ambayo inaweza kuendelea kutoa.”

Ameongeza kuwa maarifa hayo lazima pia yawe jumuishi, yakileta pamoja taaluma mbalimbali, maeneo tofauti na mitazamo mbalimbali, ikiwemo ile ya jamii za watu wa asili na jumuiya za wenyeji.

“Mwishowe, sisi sote ni sehemu ya jamii moja na lazima tupige makasia kuelekea upande mmoja… njia pekee ya kutoka katika hali hii ni kufanya kazi pamoja,” amesema Fabien Cousteau, mtetezi wa bahari na mjukuu wa mpelelezi maarufu wa bahari Jacques Cousteau, katika Klabu ya Wavumbuzi.

Balozi Bahia Tahzib-Lie, ambaye ni Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Uholanzi katika Umoja wa Mataifa, amesema kwamba tathmini hiyo “inatoa ramani madhubuti ya hatua za kuchukua kupitia ushirikiano wa kimataifa na mfumo wa ushirikiano wa mataifa mengi.”

Kama mmoja wa wenyeviti wenza wa tathmini hiyo, amesisitiza kuwa ripoti hii ya kihistoria inaweza kuwa tathmini ya bahari iliyo kamili zaidi na yenye maarifa ya kina zaidi kuwahi kufanywa hadi sasa.

Ripoti itazinduliwa rasmi kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa Juni 8 ambayo ni siku ya kimataifa ya bahari.

Soma ripoti nzima hapa

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *