Katika maadhimisho hayo yaliyofanyika Makao Makuu ya Umoja huo jijini New York Marekani Guterres alianza kwa kuweka shada la maua kuwakumbuka takriban walinda amani 4500 waliopoteza maisha wakati wakitekeleza majukumu yao tangu kuanza kwa operesheni hizo mwaka1948.

“Walinda amani wanaendelea kukabiliwa na hatari huku wakidumisha amani na tunatoa shukrani zetu za dhati kwao kwa huduma na kujitolea kwao,” amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa.

Maadhimisho haya yanalenga kutambua na kuezi ujasiri, huduma na kujitolea kwa wanajeshi, polisi na raia wanaohudumu katika shughuli za amani za Umoja wa Mataifa kote ulimwenguni. 

Maadhimisho haya kila mwaka yanatoa heshima kwa walinda amani wanaofanya kazi katika baadhi ya mazingira magumu zaidi duniani ili kuwalinda raia, kuunga mkono makubaliano ya amani na kusaidia jamii kujenga upya maisha yao baada ya migogoro. 

Katika hotuba yake Katibu Mkuu Guterres aliwashukuru walinda amani ambao wameonesha kujitolea na ushujaa wa kipekee katika wajibu wao na kuwakumbuka wale waliopoteza maisha yao walipokuwa wakihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa. 

Umoja wa Mataifa Sergii Prykhodko wa Ukraine atapewa Tuzo ya Kapteni Mbaye Diagne kwa Ujasiri wa Kipekee.

Tuzo kwa walinda amani

Sambamba na uwekaji wa shada la maua, Katibu Mkuu pia alitunuku Nishani ya Dag Hammarskjöld, Nishani ya Kapteni Mbaye Diagne ya Ujasiri wa Kipekee, Tuzo ya Afisa Polisi Mwanamke wa Mwaka na Tuzo ya Mtetezi wa Usawa wa Kijinsia.

Guterres ameitoa tuzo ya juu zaidi ya kulinda amani, Nishani ya Kapteni Mbaye Diagne kwa ujasiri wa kipekee, kwa wanajeshi wawili walioonesha kujitolea katika hatari kubwa. Mmoja wao alipokea nishani hiyo baada ya kifo chake. Mjane wake alipokea nishani hiyo kwa niaba yake.

Sergey Prikhodko,  – Nishani ya Kapteni Mbaye Diagne

Miongoni mwa waliogusa hisia za wengi katika maadhimisho hayo alikuwa rubani wa helikopta kutoka Ukraine, Sergey Prikhodko, ambaye alitunukiwa Nishani ya Kapteni Mbaye Diagne baada ya kifo chake. Mjane wake pamoja na binti yake walihudhuria hafla hiyo kupokea tuzo kwa niaba yake.

Prikhodko alipoteza maisha mwezi Machi 2025 akiwa katika operesheni ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini. Akiwa sehemu ya kikosi cha helikopta cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo (UNMISS), alijitolea kuchukua nafasi ya mwenzake mwenye uzoefu mdogo katika operesheni ya kuwaokoa wanajeshi waliokuwa wamezingirwa katika jimbo la Upper Nile.

Wakati wa operesheni hiyo, helikopta ya Umoja wa Mataifa ilishambuliwa kwa risasi licha ya kuwepo kwa dhamana za usalama, na kusababisha kifo chake pamoja na kujeruhiwa kwa wafanyakazi wengine wawili.

Akizungumza mbele ya familia yake, Guterres alisema, “Mke na binti wa Sergey wako nasi leo. Nataka mjue kuwa wakati wa huduma yake, Sergey alisaidia kuokoa maisha ya watu wengi. Alifariki akiwa katika juhudi za kuokoa maisha ya wengine zaidi. Atakumbukwa kwa muda mrefu na wenzake nchini Sudan Kusini na familia nzima ya Umoja wa Mataifa.”

Umoja wa Mataifa Sejenti Matias Reyes wa Uruguay anapokea Tuzo ya Kapteni Mbaye Diagne kwa Ujasiri wa Kipekee.

Sajenti Matias Reyes wa Uruguay – Nishani ya Kapteni Mbaye Diagne 

Nishani hiyo pia ilitolewa kwa Sajenti Matias Reyes wa Uruguay, anayehudumu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO).

Wakati wa mapigano makali mjini Goma mwezi Januari mwaka 2025, aliwaokoa wanajeshi 12 waliojeruhiwa vibaya kwa kuwahamisha kutoka eneo la mapigano hadi kituo cha matibabu chini ya mashambulizi ya risasi.

Tuzo ya Mtetezi wa Usawa wa Kijinsia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alimtunuku Meja Abhilasha Barrack wa India tuzo ya Mtetezi wa Usawa wa Kijinsia katika Jeshi. 

Akitumikia kusini mwa Lebanon, amekuwa akijumuisha masuala ya kijinsia katika operesheni za kijeshi na kusaidia zaidi ya wanawake na wasichana 5,000 kupitia elimu, maendeleo ya kitaaluma na juhudi za kupona baada ya migogoro.

Umoja wa Mataifa Meja Abhilasha Barak wa India atapokea Tuzo ya Msemaji wa Kijinsia wa Jeshi wa Mwaka.

Tuzo ya Afisa Polisi Mwanamke wa Mwaka

Tuzo ya Afisa Polisi Mwanamke wa Mwaka ilitolewa kwa Inspekta Stefanie Koenigs wa Ujerumani aliyekuwa akihudumu nchini Sudan Kusini.

Kupitia mfumo mpya wa doria aliouanzisha, alisaidia kuimarisha mifumo ya tahadhari za mapema, kufanya maamuzi wakati wa majanga na kuongeza imani ya jamii kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa.

Kwa sasa zaidi ya walinda amani 68,000 wa Umoja wa Mataifa wanaendelea kuhudumu katika operesheni mbalimbali duniani, wakilinda raia, kusaidia utekelezaji wa makubaliano ya amani na kutoa matumaini kwa mamilioni ya watu wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *