
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva Uswisi, Mwakilishi wa UNHCR nchini Sudan Kusini, Matthew Brook, ameitaja Kaunti ya Akobo kuwa ndio iliyoathirika zaidi, ambapo takribani watu 140,000 wamekimbia makazi yao. Tangu mwezi Desemba 2025, zaidi ya watu 300,000 wamefurushwa kutoka makazi yao katika Jonglei na maeneo jirani, huku wengine 100,000 wakikimbilia nchini Ethiopia kutafuta usalama.
“Timu zetu zimekuta familia nyingi zikirejea na kukuta nyumba zao zimeharibiwa au kuporwa,” amesema Brook. Ameongeza kuwa watoto wengi wameathiriwa kisaikolojia kutokana na kushuhudia ghasia, huku wanawake wakikumbwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyohusiana na mzozo huo.
UNHCR imesema ukosefu wa makazi salama, huduma za afya na misaada mingine muhimu unaongeza hatari kwa wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu.
Hali huwenda kuwa mbaya zaidi
Wakati hayo yakiendelea, kuanza kwa msimu wa mvua kunatarajiwa kuzidisha mateso ya waliokimbia makazi yao.
Mafuriko makubwa yaliyoikumba Sudan Kusini mwaka 2025 yaliathiri zaidi ya watu milioni moja na kuharibu miundombinu muhimu.
Brook ameonya kuwa bila ufadhili wa haraka, “maelfu ya familia zitakabili msimu wa mvua bila makazi salama, huduma muhimu wala ulinzi wanaohitaji ili kuendelea kuishi.”
Hadi kufikia mwezi Mei 2026, UNHCR ilikuwa imepokea asilimia 25 tu kati ya dola milioni 286 zinazohitajika kwa operesheni zake nchini humo na imetoa ombi la kupata usaidizi zaidi.