IRINGA: MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Fatma Rembo (CCM), ameibuka kuwa sauti ya wanawake wa Mkoa wa Iringa baada ya kuiomba Serikali kuanzisha benki maalumu ya wanawake itakayowawezesha kupata mitaji yenye masharti nafuu na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.
Rembo aliwasilisha hoja hiyo mbele ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kata ya Ifunda, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ikiwa ni sehemu ya hitimisho la ziara yake ya jimbo kwa jimbo mkoani Iringa.

Akizungumza kwa niaba ya wanawake wa mkoa huo, Rembo alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, akibainisha kuwa fedha hizo zimekuwa msaada mkubwa katika kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato.
Alisema zaidi ya Shilingi bilioni tatu tayari zimewanufaisha wananchi kupitia vikundi zaidi ya 600, hali ambayo imechangia kukuza shughuli za kiuchumi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Iringa.
Pamoja na mafanikio hayo, alisema wanawake bado wanakabiliwa na changamoto za kupata huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji yao, hasa wale wa vijijini ambao wengi wao hukosa taarifa sahihi kuhusu taratibu za mikopo na masharti ya taasisi za kifedha.

“Wanawake wa Iringa wamenituma kuwasilisha ombi hili. Tunahitaji benki maalumu ya wanawake au mfuko madhubuti wa uwezeshaji wa kiuchumi utakaorahisisha upatikanaji wa mitaji, kuongeza uwazi na kutoa fursa kwa wanawake wengi zaidi kushiriki katika shughuli za uzalishaji mali,” alisema Rembo.
Alieleza kuwa wananchi wengi wa kawaida, hususan wa maeneo ya vijijini, hukumbana na changamoto ya kutofahamu utaratibu wa kupata mikopo, jambo linalowafanya washindwe kutumia ipasavyo fursa zilizopo za uwezeshaji wa kiuchumi.
“Wengi hawana taarifa za kutosha kuhusu masharti ya mikopo, vigezo vinavyotakiwa wala hatua za kufuata katika mchakato wa maombi. Hali hiyo imekuwa kikwazo kwa wananchi wengi kushiriki kikamilifu katika fursa za kiuchumi,” alisisitiza.

Mbunge huyo alisema kuanzishwa kwa benki maalumu ya wanawake kutasaidia si tu upatikanaji wa mitaji, bali pia kutoa elimu ya biashara, usimamizi wa fedha na mbinu za kukuza biashara kwa ufanisi.
“Tunapozungumzia uchumi jumuishi, tunahitaji taasisi itakayowafikia wanawake wa vijijini na mijini kwa usawa. Benki hiyo itakuwa chachu ya maendeleo ya wanawake na familia zao,” alisema.
Rembo alifananisha hatua hiyo na jitihada ambazo Serikali imekuwa ikizifanya katika sekta ya kilimo kupitia ruzuku za pembejeo, huduma za ugani na uwezeshaji wa kifedha kwa wakulima, akisema mfumo kama huo unaweza kutumika kuwainua wanawake kiuchumi.
“Nina ndoto ya kuona wanawake wa Iringa wanasimama kiuchumi, wanamiliki biashara kubwa na kuwa sehemu ya nguvu ya uzalishaji wa taifa. Naamini kupitia maono ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya uchumi jumuishi, jambo hili linawezekana,” alisema.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuu Dk. Mwigulu Nchemba alisema Serikali imepokea maoni hayo na itaendelea kuyafanyia kazi kwa lengo la kuimarisha mifumo ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mkazo katika kuhakikisha makundi mbalimbali ya kijamii, hususan wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, yanapata fursa za kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na uzalishaji mali.
Mbali na hoja hiyo, Rembo alimpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho makubwa yaliyofanyika katika sekta ya afya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, akieleza kuwa uwekezaji huo umeongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.
Alisema halmashauri hiyo yenye majimbo mawili ya uchaguzi kwa sasa ina vituo vya afya 11, zahanati 81 na hospitali ya wilaya ambayo inaendelea kujengwa, huku huduma za afya ya mama na mtoto zikiendelea kuboreshwa na kuwapa wanawake maeneo salama ya kujifungulia.