Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, Mhe. Reuben Kwagilwa, amemuelekeza Mkurugenzi wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kushirikiana na Mamlaka ya Bonde la Wami/Ruvu kufanya ukaguzi upya wa viwanda vyote vinavyotiririsha maji katika mtaro unaopita eneo la Kona ya Sahala Mtaa wa Butiama, Kata ya Vingunguti jijini Dar es Salaam.

Maelekezo hayo ameyatoa kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, baada ya kufanya ukaguzi wa eneo hilo na kubaini athari za mazingira pamoja na uharibifu wa miundombinu unaodaiwa kusababishwa na utiririshaji wa maji kutoka baadhi ya viwanda.

Mhe. Kwagilwa amesema ukaguzi huo unapaswa kubaini viwanda vyote vinavyotiririsha maji katika mtaro huo na kujiridhisha kuwa maji yanayotoka viwandani yanatibiwa na kuruhusiwa kwa mujibu wa sheria kabla ya kuingia kwenye mazingira.

Aidha, amesisitiza ushirikiano wa karibu kati ya NEMC, Mamlaka ya Bonde la Wami/Ruvu na halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam husika katika kusimamia utekelezaji wa sheria za mazingira.

“Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais – Muungano na Mazingira, ninamuelekeza Mkurugenzi wa NEMC wakishirikiana na watu wa Bonde la Wami/Ruvu wafanye upya ukaguzi wa viwanda vyote ukanda huu ili wabainishe viwanda vyote vinavyotiririsha maji kwenye mtaro huu na wajiridhishe kuwa maji hayo ni safi, salama na yametibiwa kabla ya kuruhusiwa kurudi kwenye mazingira yetu,” amesema Mhe. Kwagilwa.

Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vinavyosababisha uharibifu wa mazingira na miundombinu ya umma, akitaka wahusika wote kuwajibika ili kulinda uwekezaji mkubwa uliofanywa kwa fedha za wananchi.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *