Katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inayokumbwa na mlipuko wa Ebola, juhudi kubwa za upimaji wa mapema na ufuatiliaji wa watu waliokutana na wagonjwa zinasaidia kudhibiti virusi hivyo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limesema leo Jumanne Juni 9.

Mlipuko huo unaosambaa kwa kasi, ambao pia umefika nchi jirani, Uganda, unasababishwa na aina nadra na hatari ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo. Mkurugenzi wa Operesheni za Tahadhari na Hatua za Dharura za Afya za WHO, Dkt. Abdirahman Mahamud, amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva,Uswisi kwamba kufikia jana tarehe 8 Juni, DRC ilikuwa imerekodi wagonjwa 550 walivyothibitishwa na vifo 101.

“Habari njema ni kwamba tuna wagonjwa 19 ambao wamepona hadi sasa, hivyo utambuzi wa mapema na matibabu huokoa maisha,” amesema.

Akizungumza kutoka Bunia katika jimbo la Ituri, ambalo linachangia asilimia 94 ya wagonjwa wote nchini, Dkt. Mahamud ameeleza kuwa ongezeko la wagonjwa waliothibitishwa linatokana na kuimarishwa kwa upimaji. Maabara zaidi zimefunguliwa ili kuharakisha uchunguzi wa sampuli zinazoshukiwa kuwa na Ebola, ikiwemo maabara inayofanya kazi kikamilifu katika eneo la Mongbwalu.

Nchini Uganda, wagonjwa 19 wamethibitishwa, vikiwemo vifo viwili, pamoja na mgonjwa mmoja aliyefariki akishukiwa kuwa na Ebola. WHO imesema hadi sasa hakuna ushahidi wa maambukizi ya jamii nchini humo.

© WHO/Joël Lumbala Mwitikio wa WHO dhidi ya mlipuko wa Ebola nchini DR Congo.

Uwezekano mdogo wa kuenea zaidi

Kufikia tarehe 6 Juni nchini DRC, watu 5,040 waliokuwa wamekutana na wagonjwa walikuwa wametambuliwa na kufuatiliwa katika majimbo ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini. Kuongezeka kwa juhudi za ufuatiliaji kumewawezesha wahudumu wa afya kuwafikia asilimia 62 ya watu hao, huku lengo likiwa kufikia kati ya asilimia 90 na 95 katika wiki zijazo.

Dkt. Mahamud amesema maendeleo yanafanyika hatua kwa hatua kupitia kujenga imani na kushirikiana na jamii. Amesisitiza kuwa wahudumu wa afya wa eneo husika wana mchango mkubwa katika kugundua wagonjwa mapema na kuwaelekeza kwenye vituo vya matibabu.

Ameeleza kuwa mfumo uliopo kwa sasa unafanya kazi vizuri kuanzia ufuatiliaji wa ugonjwa, ufuatiliaji wa waliokutana na wagonjwa, vituo vya matibabu hadi maabara, pamoja na ushirikishanaji bora wa taarifa.

Hata hivyo, changamoto bado zipo katika maeneo ya mbali yenye mawasiliano hafifu, ambapo sampuli zinaweza kuchukua hadi saa nane kufikishwa maabara. “Ituri ni kubwa kama Ufaransa,” amesema Dkt. Mahamud. Amebainisha kuwa wagonjwa waliopo Bunia wanaweza kupata matokeo ndani ya saa moja au mbili, lakini maeneo ya mbali zaidi yanaweza kusubiri hadi saa 24.

Katika hatua ya kutia moyo, maabara mpya katika eneo la Aru, karibu na mpaka wa Uganda, inatarajiwa kuanza kazi ifikapo Ijumaa. Hivi sasa sampuli kutoka eneo hilo hulazimika kusafirishwa kwa saa 10 kwa njia ya barabara kabla ya kupimwa.

WHO imeanzisha maabara za muda katika maeneo matano yaliyoathiriwa ili kurahisisha upimaji karibu na kitovu cha mlipuko. Kwa kushirikiana na washirika wake na kuunga mkono juhudi za serikali, shirika hilo limetuma zaidi ya wataalamu 100 nchini DRC, limewasilisha tani 40 za vifaa na bidhaa za matibabu, na kusaidia kuanzisha vituo vya matibabu ya Ebola.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *