Mechi ya kirafiki iliyopangwa kuchezwa Juni 11, 2026 baina ya Timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ na Uganda, imeahirishwa.

Taarifa ya kuahirishwa huko imetolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF).

“Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), limeusogeza mbele mchezo wa kimataifa wa kirafiki kati ya timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) dhidi ya timu ya taifa ya Uganda (Cranes), kutokana na sababu ambazo zipo nje ya uwezo wake.

“Hivyo, ZFF itaupangia tena Mchezo huo tarehe nyingine katika kipindi cha dirisha lijalo la Kalenda ya FIFA.

“ZFF inapenda kulishukuru Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) kwa utayari wake wa kushirikiana na ZFF katika kuendeleza na kukuza mchezo wa Mpira wa Miguu Zanzibar.

“Aidha pia, Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) linapenda kuwashukuru Wadau kwa mashirikiano ya dhati walioonyesha muda wote wa maandalizi ya mchezo huo,” imesema taarifa ya ZFF.

Licha ya ZFF kutotaja sababu, uwepo wa kundi kubwa la wachezaji wa timu zinazoshiriki Ligi Kuu ya NBC katika kikosi cha Zanzibar Heroes unaonekana kuchangia kufutwa kwa mchezo huo.

Kati ya wachezaji 26 walioitwa katika kikosi hicho kwa ajili ya mechi hiyo, 17 ni wa klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya mapumziko ya wiki mbili kupisha kalenda ya FIFA, imepangwa kurejea tena, Juni 12, 2026.

Inaripotiwa kwamba klabu za Simba, Azam na Yanga hazijatoa ruhusa kwa wachezaji wao walioitwa katika kikosi cha Zanzibar Heroes.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *