
JE, atatoboa? Hilo ndilo swali ambalo kwa sasa linazunguka vichwani mwa mashabiki wa Simba na wadau wa soka nchini baada ya kipa wa klabu hiyo Moussa Camara kuanza kuonyeshwa njia ya kuelekea Ulaya, huku klabu ya FC Annecy ya Ufaransa ikitajwa kuwa karibu kunasa saini yake.
Camara alikuwa mmoja wa makipa bora katika Ligi Kuu Bara kwa misimu ya karibuni, amepokea ofa ya miaka miwili kutoka FC Annecy inayoshiriki ligi ya pili nchini Ufaransa. Mbali na ofa hiyo, kipa huyo pia anafuatiliwa na klabu moja kutoka Kazakhstan, lakini taarifa zinaeleza kuwa mazungumzo na Annecy yamefikia hatua nzuri zaidi.
kipa huyo alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu wa 2024/25 akitokea Guinea na hakuchukua muda mrefu kuonyesha uwezo wake. Mara baada ya kutua Msimbazi alifanikiwa kujihakikishia nafasi ya kipa namba moja, akiwaacha benchi makipa waliokuwa wamezoeleka kikosini hapo kama Aishi Manula.
Katika msimu wake wa kwanza akiwa Simba, Camara aligeuka kuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi ndani ya kikosi hicho kutokana na uwezo wake wa kuokoa mipira ya hatari, kuongoza safu ya ulinzi na utulivu wake katika mechi kubwa, jambo lilomfanya aongezewe mkataba wa mwaka mmoja tena, ambao unamalizika mwishoni mwa msimu huu ingawa aliutumikia akiwa nje kutokana na majeraha.
HISTORIA INAMKATAA
Hata hivyo, historia ya wachezaji waliotoka Tanzania kwenda Ufaransa imekuwa na sura mbili tofauti. Wapo walioondoka na ndoto kubwa, lakini wakashindwa kung’ara kama ilivyotarajiwa.
Mfano mzuri ni Pape Sahko na Shomari Kapombe ambao waliwahi kujaribu bahati yao nchini humo, lakini safari zao hazikuzaa matunda makubwa kama wengi walivyotarajia.
Pia upande wa mafanikio ambao unaweza kumpa matumaini Camara. Mastaa waliowahi kucheza katika ligi za Afrika Mashariki na baadaye kutoboa Ulaya kama Shabani Nonda na Mbwana Samatta walionesha kuwa inawezekana kwa mchezaji kutoka ukanda huu kwenda kushindana katika kiwango cha juu kabisa.
MSALA UPO SIMBA
Kwa upande wa Simba, suala la Camara limeibua mjadala mkubwa ndani ya klabu hiyo kutokana na umuhimu wake katika kikosi hicho. Mwanaspoti liliwahi kuandika namna mabosi wa Simba walivyokuwa wakitafuta mbadala wa muda mrefu langoni, jambo lililoonyesha namna nafasi ya kipa ilivyokuwa nyeti ndani ya kikosi hicho.
Licha ya baadhi ya viongozi wa Simba kutamani kumuona akiendelea kubaki Msimbazi, hadi sasa hakuna mkataba mpya uliowasilishwa kwa kipa huyo jambo ambalo limefungua milango kwa timu zinazomuhitaji.
Mwen yekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crescentius Magori aliwahi kuliambia Mwanaspoti kuwa, Simba itafanya uamuzi ya kipa gani wanakwenda naye msimu ujao kutokana na mapendekezo ya kocha mkuu wa kikosi hicho Steven Barker.
Nafasi ya Camara Simba inazidi kuwa ndogo kwani kocha Barker amefanya kazi na Djibrilla Kassali ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu, huku rekodi zake zikizidi utamu akiwa na clean sheets 12.
KWA UPANDE WA CAMARA
Msimamizi wa Camara amesema wazi kuwa mchezaji huyo hawezi kuendelea kusubiri bila uhakika wakati kuna fursa kubwa zinazomsubiri nje ya Tanzania.
“Simba hawajampa mkataba wowote Camara, wapo viongozi ambao wanatamani abaki, tunaiheshimu Simba lakini Camara ni kipa mzuri hawezi kusubiri uamuzi ya Simba,” alisema msimamizi huyo ambaye hakutaka kutajwa.
Aliongeza kuwa kwa sasa kila kitu kinasubiri uamuzi wa mwisho wa kipa huyo mara baada ya kurejea kutoka majukumu ya timu yake ya taifa.
“Kwasasa tunasubiri arudi timu ya Taifa ili aweze kufanya uamuzi, tumeshapokea nakala ya mkataba kutoka Ufaransa kwa timu ya FC Annecy, mazungumzo yetu yanaendelea vizuri sana tunaamini atakwenda huko kwa msimu ujao.”
Iwapo dili hilo litakamilika, Camara atakuwa miongoni mwa makipa wachache waliotoka Ligi Kuu Tanzania kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya. Swali kubwa linalobaki ni moja tu; je, atafuata nyayo za waliokwama au atajiunga na orodha ya nyota waliotoboa na kuandika historia mpya nje ya mipaka ya Afrika?