
Leo ni Jumatatu 22 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1447 Hijria sawa na 8 Juni 2026.
Katika siku kama ya leo miaka 1387 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, Maytham al-Tammar mmoja wa Masahaba na wafuasi wa Mtume Muhammad (saw) aliuawa shahidi.
Awali Maytham al-Tammar alikuwa mtumwa na alinunuliwa na kuachiwa huru na Imam Ali bin Abi Talib (as). Imam Ali alikuwa akimpenda na kumthamini sana Maytham al-Tammar kama ambavyo Maytham pia alikuwa na mapenzi makubwa kwa Imam Ali.
Hatimaye katika siku kama ya leo, sahaba huyo mwema wa Mtume (saw) aliuawa kinyama na watawala wa Bani Umayyah kwa kosa la kuwapenda na kuwatetea Ahlul Bait (as). ***
Siku kama ya leo miaka 966 iliyopita alifariki dunia malenga na arifu mkubwa wa Kiislamu na wa Iran wa karne ya tano Hijria, Khaja Abdullah Ansari.
Alizaliwa katika mji wa Herat ulioko Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat.
Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi, mashuhuri zaidi vikiwa ni “Munajat Nameh”, “Mohabbat Nameh” na “Zadul Arifin”. Vilevile ameandika tafsiri ya Qur’ani Tukufu aliyoipa jina la “Kashful Asrar.” *****
Siku kama ya leo miaka 196 iliyopita inayosadiafiana na tarehe 8 Juni 1830, Camberz mbunifu wa Kijerumani alivumbua utengenezaji wa kiberiti.
Tofauti kubwa ya kiberiti hicho cha awali na hiki kinachotumiwa hivi sasa, ni uwakaji wake uliokuwa wa taratibu. Baada ya Camberz walijitokeza watafiti wengine kadhaa waliofanya utafiti wao kuhusiana na kiberiti, na hatimaye Phillips raia wa Kimarekani alifanikiwa kutengeneza kiberiti kama hiki ambacho kinatumika leo hii. ***
Tarehe 8 Juni miaka 171 iliyopita, Lisbon mji mkuu wa Ureno uliharibika kutokana na mtetemeko mkubwa wa ardhi na moto uliosababishwa na zilzala hiyo.
Karibu wakazi arubaini elfu (40,000) wa mji huo walipoteza maisha yao na thuluthi mbili ya nyumba na taasisi za kiuchumi za mji huo zilibomolewa. Mbali na maafa hayo, karibu meli elfu mbili, boti na ngarawa (ngalawa) nyingi zilizokuwa katika bandari za Ureno zilizama. Mtetemeko huo ni moja ya mitetemeko mikubwa zaidi ya ardhi kuwahi kuikumba Ureno. ****
Siku kama ya leo miaka 33 iliyopita, shirika la ujasusi la utawala haramu wa Kizayuni wa Israel, Mossad, lilifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya kiongozi mwingine wa Kipalestina katika moja ya nchi za kigeni.
Siku hiyo maajenti wa Mossad walimuuwa Atef Bseiso mmoja wa viongozi wa usalama wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO huko Paris, Ufaransa.
Licha ya kwamba hakukuwepo shaka juu ya kuhusika utawala wa Kizayuni katika mauaji hayo, lakini utawala huo ghasibu ulikana kufanya jinai hiyo ya kinyama kwa kuhofia hasira za walimwengu. Hata hivyo miaka saba baadaye, polisi ya Ufaransa ilitangaza kwamba shirika hilo la ujasusi la Israel Mossad ndilo lililopanga na kutekeleza mauaji hayo. ***