
Makocha waliowahi kumnoa bondia nyota wa Tanzania, Hassan Mwakinyo wamebainisha mambo matatu yaliyochangia kipigo kwa bondia huyo dhidi ya Michel Soro wa Ivory Coast.
Mwakinyo amechapwa kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya tisa akiwania ubingwa wa dunia wa IBO katika uzani wa middle, pambano lililopigwa jijini Abidjan.
Refarii Jerome Lades alilazimika kusimamisha pambano na kumpa ushindi wa TKO Soro aliyekuwa akicheza nyumbani
Katika ukurasa wake wa Instagram Mwakinyo ameyazungumzia matokeo hayo akibainisha kwamba hayatetei kwa kupoteza kwake na haumii kwa sababu huo ndiyo mchezo, kinachomuumiza ni ni yeye kuwa ‘weak’ kiasi cha kushindwa kujitetea.
“Hata namna ya upiganaji wangu haukuwa ule mliouzoea ilikuwa ni game tough (pambano gumu) ambayo niliweka bidii zangu kwenye mazoezi ya nguvu sana na ndiyo game ambayo nilicheza nikiwa nikiwa niko weak na mwepesi sana, yote kwa yote ni matokeo na hakuna budi kupokea,” alisema Mwakinyo saa chache baada ya kipigo hicho.
Hapa nchini, baadhi ya waliowahi kuwa makocha wake kwa nyakati tofauti wameelezea kipigo kuchangizwa na mambo matatu ambayo wanaamini ndiyo yaliyomkwamisha bondia huyo namba mbili nchini kwenye uzani middle na wa 35 duniani.
Kocha Kanda Kabongo aliyemnoa Mwakinyo kwenye pambano la mwisho kabla ya kuzichapa na Soro jana amesema dalili za kupoteza kwa bondia huyo zilianza kuonekana siku ya kupima uzani ili kupanda ulingoni.
“Niliiona dosari hiyo kabla ya pambano, siku anapima uzito alikuwa weak (hakuwa imara) alipaswa kupigania uzani wa middle (kg 72), lakini wakati anapima haukufika, alikuwa na uzani wake wa zamani wa super welter (kg 68) katika ngumi hilo ni tatizo,” amesema.
Amesema hiyo ni sehemu ambayo alifeli kipindi cha maandalizi, hakuweza kusalia kwenye uzani wake aliotakiwa kupigania hivyo kusababisha kutokuwa imara ulingoni.
“Mpinzani anapojua amekuzidi uzani anaweza kufanya anavyotaka ulingoni,sababu utakuwa hauna uimara unaostahili, huna nguvu ndicho kilimkuta Mwakinyo, japo alijaribu kudeliver some punch (alipiga baadhi ya ngumi) lakini nazo hazikuwa na madhara kwa mpinzani wake,” amesema Kabongo.
Ally Mwazoa aliyewahi kuwa promota wa bondia huyo amesema alichokikosea Mwakinyo ni kucheza tofauti na aina ya upiganaji wake wa siku zote.
“Alicheza mchezo wa kurudi nyuma, kitu ambacho akikifanya huwa hana ujanja wa kutoka kwenye kona, ndicho kilichotokea na ukizingatia mpinzani wake (Soro) ana mikono mirefu,” amesema.
Amesema mchezo wa Mwakinyo huwa ni kumvaa bondia na kupigana kwa kufuata, lakini kwenye pambano la jana alicheza akirudi nyuma.
Amesema mchezo wa ngumi pia ni mchezo wa kuhamasishwa, jambo ambalo kwa Mwakinyo alionekana kuikosa.
“Mwakinyo alihitaji sapoti hata ya kambi kutokana na ukubwa na rekodi ya bondia aliyecheza naye, inawezekana Mwakinyo na Soro waliwahi kufanya sparing (mazoezi ya kupigana ana kwa ana) wanajuana na Mwakinyo alikuwa na hofu ya kucheza naye, lakini angepata hamasa bila shaka angefanya vizuri,” amesema Mwazoa.
Kocha aliyemnoa Mwakinyo kabla ya pambano hilo, Amos Martin (Amoma) amesema bondia kucheza ugenini kuna vitu vingi ikiwamo hujuma huwa vinatokea.
“Nimeongea nao kuna taarifa ambayo sio rasmi kwamba chumba chao cha kubadilishia nguo kilipuliziwa dawa, nawasubiri warudi ili tufahamu nini kilitokea,” amesema.
Kocha huyo ambaye ndiye ilikuwa aambatane na Mwakinyo kwenye pambano hilo amesema alikwama kutokana na mazingira ya kazi zake kwa muajiri, lakini msafara wa bondia huyo ulikuwa na watu wengine wanne kutoka Tanzania walioambatan naye.
“Baada ya mimi kushindwa kwenda Mwansasu ndiye alisimama kama second (msaidizi wa ulingo) wake kule, sijui nini kilitokea japo kwa taarifa zisizo rasmi nimeambiwa chumba cha kubadilishia nguo kilipuliziwa dawa, hivyo nasubiri warudi tufanye tathimini ndipo nitakuwa na nafasi ya kuzungumzia hilo,” amesema Amoma.
Kipigo hicho huenda kikapunguza nyota za Mwakinyo ambaye sasa ana tatu na nusu na kumpandisha zaidi mpinzani wake ambaye ni bondia namba moja nchini kwake na namba 11 duniani kwenye uzani wa middle anayemiliki nyota nne.
Mara ya mwisho Mwakinyo kupigwa kwa TKO ilikuwa ni Septemba 3, 2022 alipopigwa na Liam Smith, hakuwahi kupigwa tena hadi jana alipokutana na kipigo kama hicho na kuweka rekodi ya kupigwa mara nne moja kwa pointi na mengine matatu kwa KO/TKO.