
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewasilisha bajeti ya Sh8.5 trilioni kwa mwaka wa fedha 2026/27, ikipendekeza kuongeza kodi na tozo katika bidhaa na huduma mbalimbali, zikiwamo nywele bandia, pombe, maua bandia, tiketi za viwanja vya michezo na huduma za bandari.
Lakini, imetoa nafuu za kodi kwa watu wenye ulemavu, viwanda vidogo na vya kati pamoja na sekta ya mafunzo ya ufundi.
Akisoma hotuba ya bajeti hiyo leo, Alhamisi Juni 11, 2026, mbele ya Baraza la Wawakilishi, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Juma Malik Akil, amesema makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka ujao yameongezeka kwa Sh1.5 trilioni, sawa na ukuaji wa asilimia 22.11 ikilinganishwa na bajeti ya Sh6.9 trilioni ya mwaka 2025/26.
Amesema ongezeko hilo linatokana na mageuzi ya sera za mapato, kuimarishwa kwa mifumo ya ukusanyaji wa kodi pamoja na matumizi ya mikopo nafuu ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kimkakati.
“Makadirio haya yanatokana na mageuzi ya sera na mikakati mbalimbali ya ukusanyaji wa mapato, sambamba na mikopo nafuu ya ndani, ambayo Serikali inapanga kuitumia katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa mwaka wa fedha 2026/27,” amesema Dk Malik.
Kwa mujibu wa waziri huyo, Serikali imeendelea kupunguza utegemezi wa bajeti kwa misaada ya wahisani. Kiwango cha utegemezi kinatarajiwa kushuka kutoka asilimia 4.9 mwaka 2025/26 hadi asilimia 2.8 mwaka 2026/27.
Amesema hatua hiyo inatokana na kupungua kwa misaada ya washirika wa maendeleo pamoja na mkakati wa Serikali wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani.
Katika kuendeleza usawa wa kijinsia, Serikali imetenga Sh449.8 bilioni kwa ajili ya kuimarisha ujumuishaji wa masuala ya kijinsia katika miradi ya maendeleo ili kuhakikisha rasilimali za umma zinatumika kwa ufanisi na manufaa ya maendeleo yanawafikia wananchi wote kwa usawa.
Serikali kuongeza kodi na tozo
Dk Malik amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua za kuimarisha usimamizi wa mapato kwa kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali za kodi ili kuongeza mapato, kupanua wigo wa walipakodi na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Miongoni mwa mapendekezo yaliyowasilishwa ni kutoza ushuru wa bidhaa wa asilimia 10 kwenye tiketi za kuingia viwanja vya michezo, kumbi za starehe na maeneo mengine ya burudani.
Aidha, Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo imeelekezwa kuweka mifumo ya kielektroniki ya ukataji tiketi katika viwanja vya michezo ili kuongeza uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato. Hatua hiyo inatarajiwa kuingizia Serikali Sh2.27 bilioni.
Katika sekta ya utangazaji, Serikali inapendekeza kuongeza ushuru wa bidhaa kwa kampuni za televisheni za usambazaji wa matangazo kwa njia ya kebo kutoka asilimia tano hadi saba ili kuoanisha kiwango hicho na kinachotozwa Tanzania Bara.
Marekebisho hayo yanatarajiwa kuongeza mapato ya Sh1.27 bilioni.
Kwa upande wa magari, Serikali imependekeza kuanza kutoza ushuru wa bidhaa kwa magari yenye injini chini ya ujazo wa CC 1,000 ili kuleta usawa katika mfumo wa kodi. Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mapato ya Sh1.75 bilioni.
Pia, kiwango cha tozo ya uingizaji wa pikipiki kinapendekezwa kuongezwa kutoka Sh30,000 hadi Sh50,000 kwa kila pikipiki.
Ada za bandari na usafiri wa anga zapanda
Katika jitihada za kuongeza mapato ya sekta ya usafiri, Serikali imependekeza kuongeza ada za huduma za bandari kwa wasafiri wanaotumia usafiri wa baharini kati ya Unguja na Pemba, pamoja na kati ya Zanzibar na Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, ada ya huduma za bandari kwa wasafiri kutoka Zanzibar kwenda Tanzania Bara itaongezeka kutoka Dola mbili hadi Dola tatu za Marekani, huku ada kwa wasafiri kati ya Unguja na Pemba ikiongezeka kutoka Dola moja hadi Dola mbili.
Hatua hiyo inatarajiwa kuingiza Sh1.75 bilioni katika mapato ya Serikali.
Katika sekta ya usafiri wa anga, Serikali imependekeza kuongeza kodi ya miundombinu kwa abiria wanaosafiri kwa ndege kutoka Sh2,000 hadi Sh4,000 kwa kila abiria ili kusaidia kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa anga nchini.
Nywele bandia, vipodozi, maua kodi juu
Serikali pia imepanga kuongeza ushuru wa bidhaa kwa baadhi ya bidhaa zisizo za msingi, ikiwamo nywele bandia, kope bandia, kucha bandia na bidhaa zinazofanana nazo.
Kwa mujibu wa Dk Malik, matumizi ya bidhaa hizo yameongezeka kwa kiasi kikubwa katika miaka ya karibuni, hivyo ushuru wa bidhaa unapendekezwa kuongezwa kutoka asilimia 25 hadi 30.
Hatua hiyo pekee inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh1.37 bilioni.
Vilevile, ushuru wa bidhaa kwa vipodozi unapendekezwa kuongezwa kutoka asilimia 10 hadi 15.
Kwa upande wa maua, majani na matunda bandia yanayotengenezwa kwa vifaa visivyoharibika kirahisi, Serikali imependekeza ushuru wa asilimia 20 kwa maelezo kuwa bidhaa hizo huchangia ongezeko la taka na uharibifu wa mazingira.
Katika hatua nyingine, Serikali imependekeza ushuru wa asilimia 20 kwa mashine za kukausha kucha zinazotumia mionzi ya Ultra Violet (UV) au LED, ikieleza kuwa matumizi yake yanaweza kuwa na athari za kiafya kwa watumiaji.
Pombe, sigara, soseji zaguswa
Katika bajeti hiyo, Serikali imependekeza kuongeza ushuru wa bidhaa kwa pombe, mvinyo, bia na sigara.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, ushuru wa bidhaa kwa vinywaji vikali utaongezeka kutoka Sh6,000 hadi Sh7,000 kwa lita, huku ushuru wa mvinyo ukiongezwa kutoka Sh6,000 hadi Sh7,000 kwa lita.
Kwa upande wa bia, ushuru utaongezeka kutoka Sh803 hadi Sh1,500 kwa lita, wakati ushuru wa sigara utaongezeka kutoka Sh55,896 hadi Sh65,000 kwa kiwango kilichowekwa na Serikali.
Serikali imeeleza kuwa marekebisho hayo yanatarajiwa kuongeza mapato ya Sh1.25 bilioni, fedha zitakazotumika kuboresha huduma za afya.
Aidha, ushuru wa Sh500 kwa kila kilo unapendekezwa kwa uingizaji wa soseji na bidhaa zinazofanana nazo ili kudhibiti matumizi ya bidhaa hizo nchini.
Nafuu za kodi kwa wenye ulemavu
Wakati Serikali ikiongeza kodi katika baadhi ya maeneo, pia imependekeza misamaha na nafuu mbalimbali za kodi kwa sekta zinazochochea ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi.
Kwa watu wenye ulemavu, Serikali imependekeza kuondoa kodi ya miundombinu kwa uingizaji wa viti mwendo, viungo bandia, vifaa vya kusaidia kuona na kusomea, fimbo nyeupe pamoja na vifaa maalumu vya matumizi yao.
Kwa upande wa mafunzo ya ufundi na ujuzi wa amali, imependekeza kupunguza Tozo ya Kuendeleza Ujuzi (SDL) kutoka asilimia nne hadi asilimia tatu ili kuwahamasisha vijana wengi zaidi kupata mafunzo na kujiajiri.
Aidha, wawekezaji wa viwanda vidogo na vya kati ambao hawajasajiliwa katika Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) wanatarajiwa kunufaika na unafuu wa kodi katika uingizaji wa malighafi.
Dk Malik amesema hatua hiyo inalenga kuchochea uwekezaji, kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa Zanzibar.
Kubana matumizi mabaya ya misamaha
Katika kukabiliana na matumizi mabaya ya misamaha ya kodi, Serikali imesema itaunda timu maalumu ya wataalamu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), kufuatilia matumizi ya misamaha inayotolewa kwa wawekezaji na miradi mbalimbali.
Amesema baadhi ya bidhaa zinazoingizwa kwa misamaha ya kodi zinatumika kinyume cha malengo yaliyokusudiwa, hali inayopunguza mapato ya Serikali.
Kwa mujibu wa waziri huyo, hatua za kudhibiti matumizi mabaya ya misamaha zinatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh5.72 bilioni.
Akizungumzia hali ya deni la Zanzibar, Dk Malik amesema hadi Machi 31, 2026, deni la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar limefikia Sh3 trilioni.
Kati ya kiasi hicho, Sh2.987 trilioni ni deni la ndani, huku Sh14.6 bilioni ikiwa ni deni la nje.
“Hali halisi inaonesha kuwa deni la Zanzibar bado ni himilivu. Serikali inaweza kuendelea kukopa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo yenye tija na inayochangia ukuaji wa uchumi,” amesema.
Mbali na hatua hizo, Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha mifumo ya kidijitali ya ukusanyaji wa mapato, matumizi ya takwimu rasmi, uwekezaji katika teknolojia za mawasiliano na kuimarisha sekta ya nishati ili kusaidia ukuaji wa uchumi na kuongeza mapato ya ndani.