DODOMA:Kiwango cha ukosefu wa ajira nchini kimeshuka hadi asilimia 6.2 mwaka 2024 kutoka asilimia 8.7 mwaka 2020/21, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema.

Akiwasilisha Bungeni Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2025 pamoja na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2026/27, Profesa Mkumbo alisema takwimu hizo zinaonyesha kuimarika kwa mazingira ya uzalishaji, biashara na uwekezaji nchini.

Alisema wastani wa ukuaji wa ajira kwa mwaka umeongezeka hadi asilimia 7.8 mwaka 2024 kutoka asilimia 2.3 mwaka 2020/21, hatua inayodhihirisha kuongezeka kwa fursa za ajira katika sekta mbalimbali za uchumi.

“Ukosefu wa ajira umepungua kutoka asilimia 8.7 mwaka 2020/21 hadi asilimia 6.2 mwaka 2024, huku wastani wa ukuaji wa ajira kwa mwaka ukiongezeka hadi asilimia 7.8,” alisema Profesa Mkumbo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, nguvu kazi nchini imefikia watu milioni 27.3, sawa na asilimia 73.2 ya wananchi wenye uwezo wa kufanya kazi, ikilinganishwa na asilimia 72.1 mwaka 2020/21.

Kati ya watu hao, milioni 25.6 wanajishughulisha na shughuli za uzalishaji au wana ajira zinazowaingizia kipato. Sekta ya kilimo inaendelea kuajiri watu wengi zaidi kwa asilimia 54.2 ya wenye ajira, ikifuatiwa na sekta ya huduma yenye asilimia 35.5 na sekta ya viwanda yenye asilimia 10.3.

Profesa Mkumbo alisema kuongezeka kwa ajira kunatokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali kuboresha mazingira ya biashara, kuvutia uwekezaji na kuongeza shughuli za uzalishaji katika sekta mbalimbali za uchumi.

Aliongeza kuwa mwenendo huo unaonyesha mafanikio ya jitihada za Serikali katika kupanua fursa za ajira na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *