Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama barabarani Mkoani Arusha limeendelea kuimarisha mikakati ya kuzuia ajali za barabarani kwa kukutana na mawakala wa mabasi wanaotoa huduma za usafiri wa abiria ndani na nje ya Mkoa huo.

Akizungumza mara baada ya kikao hicho leo, Mkuu wa Kikosi hicho Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Zauda Mohamed amesema wamekutana na mawakala hao kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani zinazingatiwa wakati wote.

ACP Zauda amebainisha kuwa kutokana na uwepo wa vituo vya mabasi maeneo mbalimbali mkoani humo, kupitia kikao hicho wameweka mpangokazi mzuri wa kukagua mabasi hayo pamoja na madereva kabla ya kuanza safari.

Pia amesema amesema kuwa ushirikiano wa karibu baina yao na wakala wa mabasi utasaidia kuondoa changamoto zinazowakabili abiria kwa wakati, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha huduma ya usafiri inatolewa kwa kuzingatia usalama.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala Mabasi Mkoa wa Arusha (CMM) Bw. James Leonard amesema wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutekeleza maelekezo yaliyotolewa na kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia kuimarisha usalama barabarani.

Aidha, ametoa wito kwa mawakala wenzake kuhakikisha mabasi yote yanayotarajiwa kuanza safari yanakuwa katika hali nzuri kiufundi na yanaendeshwa na madereva wenye weledi ili kuhakikisha usalama wa abiria na safari zenye utulivu wakati wote.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *