
Dar es Salaam. Katika historia ya Uislamu, msikiti haukuwa tu mahali pa kuswali. Ulikuwa moyo wa jamii, kitovu cha mshikamano, darasa la elimu, mahakama ya haki, na kimbilio la wanyonge.
Leo hii, katika maeneo mengi, misikiti imebaki kuwa sehemu za kutekeleza ibada ya swala pekee, huku jukumu lake la kijamii likizidi kufifia.
Ni wakati wa kujiuliza kwa dhati: je, misikiti yetu inawajua waumini wake? Je, inatambua wajane, yatima, walemavu na wahitaji wanaoishi mita chache kutoka milango yake?
Katika hali ya sasa, misikiti mingi haijui hata idadi ya Waislamu wanaoishi katika eneo lake. Hakuna takwimu za familia zenye uhitaji maalum, hakuna orodha ya wajane wanaohitaji msaada wa kimaisha, hakuna utambuzi wa vijana waliokata tamaa au walioko kwenye hatari ya kujiingiza katika maovu.
Msikiti unafunguliwa wakati wa swala, waumini wanaingia, wanaswali na kuondoka. Uhusiano unabaki kuwa wa haraka na wa juu juu. Hakuna mfumo wa kufuatilia hali za waumini, wala jukwaa la kuzijadili changamoto zao kwa pamoja.
Wajane wengi katika jamii zetu wanabeba mizigo mizito kimya kimya. Yatima wanakua bila uangalizi wa karibu wa kijamii. Walemavu wanajikuta wamesahaulika, hata miundombinu ya misikiti mingine haiwazingatii kwa kuwajengea mazingira rafiki. Lakini misikiti ipo katikati ya mitaa yao.
Hili ni pengo kubwa kati ya dhamira ya Uislamu na uhalisia wa leo. Dini inasisitiza kuwajali wahitaji, lakini taasisi kuu ya dini katika jamii
yaani msikiti, imejikita zaidi katika ibada kuliko huduma ya kijamii.
Msikiti wa Mtume
Tukirudi katika historia, tunaona picha tofauti kabisa kupitia Msikiti wa Mtume ulioko Madina, Al-Masjid an-Nabawi. Msikiti huu haukuwa tu sehemu ya kuswali, bali ulikuwa makao makuu ya dola ya Kiislamu.
Ndani yake, Mtume Muhammad (Rehema na amani zimshukie) aliongoza mikutano ya kijamii, alipokea wajumbe kutoka makabila mbalimbali, alitoa hukumu za kisheria, na kupanga mikakati ya kulinda na kuendeleza jamii ya Waislamu. Masuala ya kiuchumi, kijamii na kisiasa yalijadiliwa hapo hapo.
Katika msikiti huo, kulikuwa na kundi la watu waliokuwa wakijulikana kama Ahlus-Suffah yaani maswahaba maskini waliokuwa hawana makazi wala mali. Waliishi katika eneo la msikiti, wakipewa malezi, chakula na elimu.
Hii ilikuwa ishara tosha kwamba msikiti haukuwa na mipaka ya ibada pekee, bali ulikuwa hifadhi ya kijamii. Hakuna aliyekuwa akilala njaa bila jamii kujua. Hakuna mjane au yatima aliyekuwa nje ya uangalizi wa umma.
Msikiti wa Mtume pia ulikuwa chuo. Maswahaba walijifunza Qur’ani, hadithi na maarifa ya maisha humo humo. Vijana walipata mafunzo ya maadili na uwajibikaji. Wanawake walikuwa na nafasi ya kuuliza maswali na kushiriki katika masuala ya kijamii. Kwa maneno mengine, msikiti ulikuwa shule, ofisi ya ustawi wa jamii, na kituo cha maamuzi kwa wakati mmoja.
Leo hii, tuna misikiti mizuri yenye majengo ya kuvutia na minara mirefu, lakini je, ndani yake kuna mifumo ya kusaidia jamii? Je, kuna kamati maalum za kutembelea wagonjwa, kufuatilia familia zenye migogoro, au kusaidia vijana kupata ajira?
Je, kuna hazina za kusaidia ada za yatima au mitaji midogo kwa wajane? Mara nyingi, michango hukusanywa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati, lakini michango ya kuendeleza maisha ya watu inakuwa midogo au isiyo na uratibu wa kudumu.
Tufanye haya
Ili misikiti irudi kuwa vituo vya kuutumikia umma, kunahitajika mabadiliko ya kimtazamo na kiutendaji. Kwanza, kila msikiti unapaswa kuwa na takwimu za waumini wake.
Misikiti ijue ni familia ngapi zipo, changamoto zao ni zipi, na ni rasilimali gani zinahitajika. Pili, kuwe na kamati za ustawi wa jamii zitakazoshughulikia moja kwa moja masuala ya wajane, yatima, walemavu na wahitaji wengine.
Tatu, misikiti iwe na programu za elimu ya maisha kwa vijana, mafunzo ya ndoa, na hata semina za ujasiriamali.
Viongozi wa misikiti wanapaswa kuona jukumu lao likizidi lile la kutoa khutba za Ijumaa pekee. Wanapaswa kuwa wasimamizi wa ustawi wa kijamii, washauri wa familia, na waunganishi wa rasilimali ndani ya jamii.
Ushirikiano na taasisi nyingine za kijamii unaweza kuimarisha huduma hizi. Msikiti unaweza kuwa daraja kati ya matajiri na maskini, kati ya wenye elimu na wasio na elimu, kati ya wenye nguvu na wanyonge.
Zaidi ya yote, ni lazima kurejesha roho ya uwajibikaji wa kijamii miongoni mwa waumini wenyewe. Msikiti si jengo tu; ni watu.
Ikiwa kila muumini atahisi kuwa ana jukumu la kumjua jirani yake, kumtembelea mgonjwa, au kumsaidia yatima, basi msikiti utarejea kuwa kitovu cha mshikamano.
Historia inatufundisha kwamba ustaarabu wa Kiislamu ulijengwa juu ya misingi ya mshikamano na huduma kwa jamii, si ibada ya peke yake.
Tukirejesha misikiti katika nafasi yake halisi kama vituo vya kuutumikia umma, tutajenga jamii imara, yenye huruma, na inayojali kila mmoja. Huo ndio urithi wa Msikiti wa Mtume, na huo ndio wajibu wetu leo.