
Wanawake na wasichana wanawakilisha asilimia 53.4 ya wagonjwa wa Ebola waliothibitishwa kwa vipimo vya maabara katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Uganda, sawa na wagonjwa 244 kati ya 457 kwa mujibu wa taarifa za wagonjwa katika maeneo zilikopatikana. Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake.
Taarifa inafafanua zaidi kwamba, miongoni mwa vijana balehe, wasichana walichangia zaidi ya asilimia 61 ya wagonjwa hao, yaani wagonjwa 27 kati ya 37 waliothibitishwa kwa vipimo vya maabara.
UN Women inaeleza ikisema, “uhalisia wa mlipuko huu wa sasa unafuata mwelekeo ule ule ambao historia imekuwa ikituonesha mara kwa mara: wanawake na wasichana huathirika zaidi katika milipuko ya Ebola. Maambukizi ya ugonjwa huu hufuata hali halisi za kijamii, yakisambaa kupitia majukumu ya ulezi, kazi za nyumbani, huduma za afya mstari wa mbele na taratibu za mazishi zinazowaweka wanawake na wasichana katika mawasiliano ya karibu na wagonjwa wakati wa hatua za maambukizi ya ugonjwa.”
Hali hii ilishuhudiwa pia katika mlipuko wa Ebola wa mwaka 2018–2019 nchini DRC, ambapo wanawake na wasichana walichangia takriban theluthi mbili ya visa vilivyoripotiwa. Hata mwaka 1976 nchini humo, wanawake walikuwa asilimia 56 ya watu wote waliofariki kutokana na ugonjwa huo.
Mlipuko wa Ebola yenye virusi vya Bundibugyo (BVD) visivyo na chanjo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaendelea kubadilika kwa kasi, huku idadi ya maambukizi na maeneo yaliyoathiriwa ikiendelea kuongezeka. Tangu kuripotiwa mlipuko wa sasa Mei 15 hadi Kufikia tarehe 10 Juni, kulikuwa na jumla ya visa 676 vilivyothibitishwa, vikiwemo vifo 136, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kufikia tarehe 11 Juni, Uganda ilikuwa imeripoti visa 19 vilivyothibitishwa, vikiwemo vifo viwili, pamoja na kisa kimoja kinachoshukiwa ambacho pia kimesababisha kifo.
Uganda haijaripoti visa vipya katika siku sita zilizopita. Mamlaka za kitaifa katika nchi hizi mbili zilizoathiriwa, kwa ushirikiano na Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na washirika wake, zinaendelea kutekeleza hatua pana za kukabiliana na mlipuko huo.
Aidha, mfumo wa kikanda wa maandalizi na upangaji wa vipaumbele unaendelea kuongoza shughuli za utayari katika nchi mbalimbali za Kanda ya Afrika.