
Dar es Salaam. Wakati habari za msanii na mfanyabiashara, Wema Sepetu kupata mtoto zilipoanza kusambaa hivi karibuni, wengi walibaki na swali moja kubwa ni kwa namna gani watu wake wa karibu waliweza kuhifadhi siri hiyo kwa miezi yote bila kuizungumza hadharani?
Kwa muda mrefu, Wema alikuwa akizungumza wazi kuhusu ndoto yake ya kuwa mama. Alipitia vipindi mbalimbali vya matumaini na majaribu huku mashabiki wake wakiendelea kumwombea.
Ndiyo maana taarifa za kujifungua kwake zilipowafikia wengi, ziliibua mshangao mkubwa kwa sababu licha ya kuwepo kwa tetesi za mara kwa mara, hakuwahi kuthibitisha ujauzito wake hadharani.
Japo kulikuwa na uvumi uliokuwa ukisambaa kwenye mitandao ya kijamii, Wema mwenyewe hakuwahi kuzungumzia suala hilo na hata marafiki zake wa karibu walibaki kimya hadi alipojifungua Juni 12, 2026.
Miongoni mwa waliokuwa karibu naye katika safari hiyo ni Aunt Ezekiel, Jacqueline Wolper, Irene Uwoya, Kajala Masanja na wengine wengi. Licha ya ukaribu wao na Wema, waliamua kuheshimu faragha yake na kutunza siri hiyo hadi wakati ulioonekana kuwa sahihi.
Aunt Ezekiel: Niliheshimu safari yake
Ni mmoja wa marafiki wa muda mrefu wa Wema ambaye mara kadhaa aliwahi kueleza imani yake ni siku moja rafiki yake angebarikiwa kupata mtoto.
Anasema kwa muda mrefu alikuwa akiendelea kumwombea na kumpa moyo, akiamini kila jambo lina wakati wake na siku moja ndoto yake ya kuwa mama ingetimia.
“Nilikuwa naamini wakati wa Mungu ni wakati sahihi. Nilijua tu siku moja Wema angekuwa mama,” anasema Aunt Ezekiel.
Anasema imani hiyo ndiyo iliyomfanya aheshimu faragha ya rafiki yake na kutotoa maelezo yoyote hadharani kuhusu ujauzito huo.
“Siyo kila kitu ambacho mtu anakitamani kukipata lazima kiwekwe hadharani. Wakati mwingine siri huficha mambo mengi na kumpa mtu amani ya moyo. Niliona ni bora kusubiri wakati sahihi,” anasema.
Jacqueline Wolper: Mwenye habari ndiye huamua wakati wa kuizungumza
Kwa upande wake, ukaribu na Wema ulimfanya kuwa miongoni mwa watu waliokuwa karibu naye katika kipindi hicho muhimu.
Hata hivyo, hakuwahi kuzungumzia jambo hilo hadharani wala kutoa ishara zozote ambazo zingeweza kuwafanya watu kubaini kilichokuwa kinaendelea.
Baada ya Wema kujifungua ndipo Wolper alianza kushiriki baadhi ya kumbukumbu na picha zilizoonyesha namna alivyokuwa akimtembelea rafiki yake nyumbani wakati wa ujauzito.
“Kuna mambo ambayo si ya kusimuliwa na marafiki. Mwenye habari ndiye anayepaswa kuamua wakati wa kuizungumza,” anasema Wolper.
Anasema kutokana na jinsi Wema alivyokuwa akitamani kupata mtoto kwa muda mrefu, haikuwa sahihi kutangaza jambo hilo kabla ya wakati.
“Kwa jinsi alivyokuwa akisubiri kupata mtoto kwa miaka mingi, tuliona ni bora kulinda furaha yake hadi kila kitu kitakapokuwa sawa,” anasema.
Irene Uwoya: Kulinda amani ya rafiki
Kwa upande wa Irene Uwoya anasema wakati mwingine urafiki wa kweli haupimwi kwa maneno mengi bali uwezo wa kuhifadhi jambo muhimu la rafiki yako.
Uwoya alikuwa miongoni mwa marafiki waliobaki karibu na Wema katika kipindi hicho bila kuzungumzia chochote hadharani licha ya maswali kutoka kwa watu mbalimbali.
“Wakati mwingine kumpenda rafiki yako ni kulinda amani yake kuliko kutafuta umaarufu kwa habari zake,” anasema Uwoya.
Anasema jambo muhimu kwao lilikuwa kuhakikisha Wema anapitia kipindi hicho kwa utulivu na furaha bila shinikizo kutoka kwa umma.
Walivyoandaa ‘baby shower’ ya kushtukiza
Mbali na kuhifadhi siri ya ujauzito huo, marafiki hao walitaka kuhakikisha Wema anapata kumbukumbu maalumu kabla ya kujifungua.
Aunt Ezekiel anasema waliamua kupanga kwa siri sherehe ya baby shower kwa ajili ya Wema bila yeye kujua ili iwe sapraiza ya kweli.
Kwa mujibu wa Aunt, marafiki na watu wa karibu walijichangisha fedha kwa pamoja na kushirikiana kupanga maandalizi yote ya tukio hilo, ambalo lilifanyika takribani wiki moja kabla ya Wema kujifungua.
“Tulijichangisha na kupanga kila kitu kwa siri. Tulitaka afurahi na ajisikie tupo pamoja naye katika safari hii,” anasema Aunt Ezekiel.
Anasema mafanikio ya tukio hilo yalitokana na ushirikiano wa watu wengi waliokuwa wanatamani kuona Wema anafurahia hatua hiyo muhimu ya maisha yake.
Siri iliyolindwa kwa upendo
Kwa wengi, simulizi za Aunt Ezekiel, Jacqueline Wolper na Irene Uwoya zinaonyesha maana halisi ya urafiki wa kweli. Badala ya kutumia taarifa walizokuwa nazo kutafuta umaarufu au kuibua mijadala kwenye mitandao ya kijamii, waliamua kusubiri hadi wakati ambao Wema mwenyewe angekuwa tayari kuishiriki furaha yake.
Hatimaye, siri hiyo ilibaki salama hadi pale Wema alipompokea mtoto wake na kutimiza ndoto aliyokuwa akiisubiri kwa miaka mingi. Nyuma ya furaha hiyo kulikuwa na marafiki walioweza kuvumilia, kunyamaza na kulinda moja ya nyakati muhimu zaidi katika maisha yake.