Dar es Salaam. Mvutano kuhusu raia wageni nchini Afrika Kusini umeingia katika hatua mpya huku maandamano ya kupinga wahamiaji yakizidi kushika kasi, hali iliyozua hofu miongoni mwa maelfu ya raia wa mataifa mengine ya Afrika wanaoishi nchini humo na kuibua misimamo mikali kutoka serikalini, makundi ya kiraia, viongozi wa dini na sekta ya biashara.

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya kimataifa kutoka nchini humo vikiwemo Radio France Internationale (RFI) na BBC, na taarifa mbalimbali za Serikali, makundi yanayopinga uhamiaji haramu yameweka Juni 30, 2026 kuwa tarehe ya mwisho wakitaka wahamiaji wote wasio na vibali kuondoka nchini humo.

Katika Jimbo la KwaZulu-Natal, maelfu ya raia wa Malawi wamekimbia makazi yao na kukusanyika katika maeneo ya umma jijini Durban wakisubiri kurejeshwa nyumbani kutokana na hofu ya kushambuliwa.

Wakati hali hiyo ikiendelea, baadhi ya mataifa ya Afrika yameanza kuchukua hatua za kuwalinda raia wao.

Ghana imerejesha mamia ya wananchi wake nyumbani kupitia operesheni iliyopewa uzito mkubwa wa kimawasiliano.

Ndani ya Afrika Kusini, mjadala huo umeibua misimamo inayokinzana, ambapo baadhi ya wananchi wanaamini ongezeko la wahamiaji, hasa wasio na vibali, limechangia ukosefu wa ajira, ushindani wa fursa za kiuchumi na kuongezeka kwa uhalifu.

Kwa upande mwingine, vyama vya wafanyakazi, viongozi wa dini na watetezi wa haki za binadamu wanasisitiza kuwa wahamiaji wanageuzwa kuwa watu wa kubebeshwa lawama kwa matatizo ya kiuchumi na kijamii ambayo yamejengwa kwa miaka mingi.

Kiongozi wa Shirikisho la Wafanyakazi wa Viwandani la Afrika Kusini (Giwusa), Mametlwe Sebei, amesema wananchi wengi wamekatishwa tamaa na kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira kinachozidi asilimia 30, lakini hasira hizo zimeelekezwa kwa watu wasiohusika.

“Tatizo si kwamba wafanyakazi wana hasira; wana kila sababu ya kuwa na hasira. Lakini wahamiaji hawakusababisha ukosefu wa ajira, kufungwa kwa viwanda, ubinafsishaji wa huduma za umma wala uporaji wa rasilimali za serikali,” amesema.

Kwa mtazamo wake, chuki dhidi ya wageni si suluhisho la matatizo ya Afrika Kusini, bali ni dalili ya mgogoro mpana wa kijamii na kiuchumi unaolikabili taifa hilo.

Mashirika ya haki za binadamu nayo yameonya dhidi ya tabia ya kuwatumia wageni kama watu wa kubebeshwa lawama kwa matatizo ambayo hayakusababishwa nao.

Viongozi wa dini pia wamejiunga katika mjadala huo. Baraza la Makanisa la Afrika Kusini (SACC), kupitia kwa Sithembele Sipuka  limesema misingi ya imani inawataka watu kuwaonyesha wageni huruma badala ya kuwafukuza au kuwanyanyapaa.

 Sipuka amesema maandiko ya kidini yanaelekeza wazi kuwapokea wageni na kuwakumbusha waumini kwamba hata watu wa Mungu waliwahi kuwa wageni katika nyakati tofauti za historia.

Wakati huohuo, sekta ya biashara imeonyesha wasiwasi wake ikihofia kwamba maandamano hayo yanaweza kuathiri uchumi wa taifa hilo na mahusiano yake ya kibiashara na mataifa mengine ya Afrika ambako Afrika Kusini ina masilahi makubwa ya uwekezaji na biashara.

Shinikizo hilo pia limeiweka Serikali ya Rais Cyril Ramaphosa katika wakati mgumu kisiasa, hasa wakati taifa hilo likielekea uchaguzi wa serikali za mitaa katika miezi michache ijayo.

Msimamo wa Serikali

Akilihutubia taifa, Jumapili Juni 7, 2026, Ramaphosa alikiri kuwepo kwa wasiwasi wa wananchi kuhusu uhamiaji haramu, lakini akakemea vikali vitendo vya chuki dhidi ya wageni na makundi yanayochochea mgawanyiko.

Alisema hakuna nafasi ya chuki dhidi ya wageni, ubaguzi wa rangi, ubaguzi dhidi ya Waafrika au aina yoyote ya vurugu nchini humo.

“Tusikubali kupotoshwa na wale wanaotaka tuwakabili wale ambao hawakuzaliwa katika ardhi yetu. Hatutaruhusu makundi kutumia wasiwasi wa wananchi kuyumbisha nchi na kuchochea utengano na vurugu,” alisema Ramaphosa.

Pamoja na msimamo huo, rais huyo alitangaza hatua za kuimarisha usimamizi wa uhamiaji, ikiwamo kuimarisha ulinzi wa mipaka, kuongeza ukaguzi wa kampuni zinazoajiri watu wasio na vibali, kuanzisha mahakama maalumu za kushughulikia wahamiaji haramu na kuongeza adhabu kwa waajiri wanaokiuka sheria za uhamiaji.

Kauli ya rais imeonyesha mizani ambayo serikali ya Afrika Kusini inalazimika kuicheza, upande mmoja ikikiri wasiwasi wa wananchi kuhusu uhamiaji haramu na upande mwingine ikikataa chuki na vurugu dhidi ya wageni.

Hali ya Watanzania waliopo Afrika Kusini

Kwa Watanzania walioko Afrika Kusini, taarifa zinazotoka nchini humo zimeendelea kufuatiliwa kwa karibu.

Mtanzania anayetumia jina la Kigz Didas kwenye mitandao ya kijamii, aliyejitambulisha kuwa anaishi nchini humo, amesema baadhi ya maeneo yameathiriwa na hali ya taharuki.

“Mimi naweza kusema sehemu zilizo salama ni ambako kuna Wazungu tu. Lakini sehemu nyingi ambazo kuna watu weusi wa asili ya Kizulu kuna vurugu. Hapa Cape Town kuna baadhi ya maeneo kazi hazifunguliwi,” ameandika mitandaoni.

Hata hivyo, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, James Bwana, amesema Watanzania wanaoishi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo wameendelea kuwa salama licha ya kuwepo kwa maandamano hayo.

“Watanzania wetu katika maeneo mbalimbali ndani ya Afrika Kusini wameendelea kuwa salama, na kama wapo watu wanaopata matatizo basi yanatokana na aina nyingine ya uhalifu na hayahusiani moja kwa moja na matukio ya maandamano,” amesema.

Hata hivyo, hali ya kiusalama nchini humo inaripotiwa kuwa ya wasiwasi kadri Juni 30 inavyokaribia. Hali inayosababisha macho ya Waafrika wengi  kuelekezwa Afrika Kusini kujua hatima ya maelfu ya ndugu zao waliopo huko.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *