UHAKIKA ni Yanga haitaendelea na winga wake Buba Jammeh baada ya kutoridhishwa na uwezo wake lakini mezani kwa mabosi wa klabu hiyo kuna mawinga watatu ambao mmoja wao atapishana na raia huyo wa Gambia.

Buba alikuja Yanga usajili wa Januari uliopita akiletwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Mreno Pedro Goncalves, lakini tangu ujio wa winga huyo ameshindwa kuingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza, akitumia muda mwingi kukaa benchi.

Mabosi wa Yanga wameanza msako mapema wa kutafuta mrithi wake na kuna majina matatu mezani kwao wote wakiwa raia wa Congo na wawili wanatoka DR Congo na mmoja akitoka upande mwingine wa Congo Brazaville.

Jina la kwanza Henoc Molia, ambaye ni raia wa DR Congo anayeichezea FC Lupopo, Yanga hesabu zao ni winga huyu ndio chaguo lao la kwanza lakini kupata saini yake kuna vita kubwa itatakiwa kupigana.

Molia ameshakubaliana karibu kila kitu na matajiri wa Chamazi, Azam FC wakimuwekea fedha za kufuru mezani, pia klabu yake imeshatajiwa kiasi ambacho itavuna kutokana na dili hilo, Yanga ili impate inatakiwa kutumia msuli mkubwa wa kifedha kubadili dili hilo.

Kocha wa Azam Florent Ibenge, huyu ndiye winga chaguo lake la kwanza na uhakika wa kumpata ndio uliomfanya pia kocha huyo kukubali kusalia ndani ya klabu hiyo akijua uhakika anaweza kuwa na timu tishio.

Yanga bado haijakata tamaa inaendelea kupigania saini ya winga huyu hatari ambaye kwa sasa kwenye ligi ya Congo ni mmoja kati ya wachezaji mahiri.

Nyuma ya Molia kuna mwingine Christian Saile Basomboli anayeichezea Siwelele FC ya Afrika Kusini, Yanga pia imefanya naye mazungumzo kwa lengo la kumsajili kama ikimkosa yule wa Lupopo.

Saile msimu uliopita ana ambao hapa kwetu bado haujamalizika amecheza jumla ya mechi 16 akitumia dakika 864, akikosa mechi 13 tu akifunga mabao manne.

Saile amekubali kutua Yanga baada ya mazungumzo na bosi mmoja wa juu wa timu hiyo akiwa na uwezo wa kucheza winga wa kulia amekuwa akitajwa kama mmoja kati ya mawinga wa kisasa kutokana na uwezo wake wa kupanda na kushuka.

Jina lingine ni Wilfrid Nkaya ambaye jamaa wiki hii amesitisha mkataba wake na ES Setif ya Algeria akiona hatari kama Waalgeria hao wataua kipaji chake kutokana na kusotea sana benchi badala ya kucheza uwanjani.

Nkaya aliwasha moto akiwa na AS Otoho ya kwao Congo Brazaville, aliwahi kuja hapa nchini msimu huu kucheza dhidi ya Azam FC kwenye mechi za Kombe la Shirikisho Afrika na alionyesha uwezo mkubwa baada ya hapo akauzwa Uarabuni.

Nkaya ameichezea Setif mechi saba pekee akitumia dakika 501, akitumia muda mwingi kukaa benchi hatua ambayo imemfanya kuwarudisha mezani mabosi wa klabu hiyo na kuomba kuondoka, Yanga imemrukia haraka ikitafuta akili ya kumchukua hata hivyo bado kuna mazungumzo yanaendelea kuhusu dau la usajili pamoja na marupurupu.

Mawinga hao watatu Yanga inapambana impate mmoja kati yao ilia je kuongeza nguvu kwenye kikosi chao kuchukua nafasi ya Buba ambaye ni wazi ataondoka mwisho wa msimu huu kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango kizuri kwenye kikosi hicho pamoja na kusajiliwa kwa mbwembwe kwenye dirisha dogo akiwa hadi sasa hana bao lolote kwenye ligi kuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *