Arusha. Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia mfanyakazi wa usafi wa baa ya Shisha Village, Lameck Mlay (30), kwa tuhuma za kumuua Husna Shabani (33) na kutupa mwili wake kwenye shimo la maji taka lililopo katika baa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Juni 15, 2026 na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, jeshi hilo linamshikilia Lameck Mlay ambaye ni mfanya usafi (baa ya Shisha Village) na mkazi wa Maji ya Chai.

“Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa kabla ya tukio hilo, mtuhumiwa na marehemu walikuwa kwenye starehe katika eneo hilo. Uchunguzi wa tukio hilo unakamilishwa na taratibu nyingine za kisheria zitafuata.”

Taarifa ya serikali za mitaa

Taarifa za awali zinadai kuwa kabla ya kifo chake, Husna alionekana akiwa na mwanaume anayedaiwa kuwa mpenzi wake.

Akizungumza baada ya kutambuliwa kwa mwili wa marehemu, Mjumbe wa serikali ya mtaa, Veronica Karani, amesema jamii inaomba haki itendeke kwa Husna na waliohusika na tukio hilo wachukuliwe hatua za kisheria.

“Tulipata taarifa za tukio hili asubuhi. Tangu Jumamosi hatukumuona tena. Alikuwa msichana anayejitegemea na aliishi peke yake. Tunachokiomba ni haki itendeke,” amesema Karani.

Kwa mujibu wa Karani, kutoka usiku kwa Husna haikuwa jambo la kushangaza kwa kuwa alikuwa akitembelea maeneo mbalimbali ya starehe nyakati za mwisho wa wiki.

Naye mmiliki wa Shisha Village, Felix Instabul, amesema taarifa za tukio hilo zilianza kuwafikia kupitia watu waliokuwa wakifahamu uhusiano kati ya marehemu na mtuhumiwa.

Istanbul alisema walipata taarifa kutoka kwa mtu aliyewafahamisha kuwa Husna ameuawa na mfanyakazi wake, ambaye inadaiwa walikuwa na uhusiano wa muda mrefu.

Aliongeza kuwa wawili hao walikuwa wakionekana mara kwa mara pamoja, jambo ambalo halikuzua mashaka yoyote kwa watu waliokuwa wanawafahamu.

Istanbul amedai kuwa nyuma ya baa hiyo kuna nyumba za kulala wageni ambapo Jumamosi walipata taarifa kwa mmoja wa watu wa karibu wa Lameck (mtuhumiwa) ambaye alimwambia amemuomba  ushauri amegombana na mpenzi wake amefariki dunia.

Kauli ya dada wa marehemu

“Aliniambia nijikaze, mdogo wako amefariki. Baada ya kusikia maneno hayo sikujitambua tena, nilipoteza fahamu,” Hiyo ni moja ya nukuu ya Salma Musa, dada wa marehemu Husna Shabani, huku akieleza kwa uchungu namna alivyopokea taarifa za kifo cha mdogo wake aliyekuwa amepotea kwa siku kadhaa.

Amesema Husna aliondoka nyumbani kwake usiku wa Ijumaa, Juni 12,2026  kama ilivyokuwa kawaida yake na tangu wakati huo hakurejea wala kupatikana kwa simu hadi pale mwili wake ulipokutwa kwenye shimo la maji taka, Jumapili Juni 14, 2026.

Salma ameeleza hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake ambako ndipo ulipo msiba wa mdogo wake (Husna).

Ameeleza kuwa wasiwasi ulianza baada ya majirani kumpigia simu Jumamosi wakimuuliza kama mdogo wake alikuwa nyumbani kwake.

“Nilianza kumpigia simu Ijumaa, lakini haikupatikana. Niliendelea kuwasiliana na majirani na viongozi wa eneo letu ili kufahamu alipo,” amesema.

Amesema akiwa bado katika harakati za kumtafuta, Jumapili alipigiwa simu na rafiki yake ambaye alikuwa muhudumu katika baa ya Shisha Village eneo la Mbauda.

“Aliniambia anamfahamu mdogo wangu na mara ya mwisho alikuwa amevaa suruali ya kijeshi. Kisha akaniambia nijikaze kwa sababu Husna amefariki. Niliposikia hivyo nilipoteza fahamu kabisa,” amesema

Baada ya kupata nafuu, Salma alielekezwa kwenda katika baa hiyo ili kupata maelezo zaidi kuhusu kilichotokea kwa mdogo wake.

“Aliniambia ungejikaza nikakuonyeshe pale kwa meneja ufunguliwe kamera, nikamwambia huyu mtoto (mtoto wangu wa kiume), maana anamjua kwani mimi nilikuwa nimechanganyikiwa, ila walivyofika pale meneja akajificha mtoto akaambiwa arudi mpaka waende watu wazima kwani yeye ni mdogo, wakati huo mwili umeshapelekwa mochwari,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *