Zikiwa zimebaki saa chache kushuhudia mchezo wa Ligi Kuu, Mbeya City dhidi ya Simba, mashabiki wameonekana kuitikia kwa wingi mpambano huo kutokana na wingi wao wanaotaka kuingia uwanjani waliopo nje ya uwanja.

Mbeya City inatarajia kushuka uwanjani saa 8 mchana kuikabili Simba, mchezo utakaopigwa katika Uwanja wa Sokoine ukiwa ni wenye kutoa mweleleo kwa timu hizo wakati ligi hiyo ikielekea ukingoni.

Simba iliyopo nafasi ya pili kwa piinti 61, inawania ubingwa ilioukosa kwa misimu minne mfululizo, huku City iliyopo nafasi ya 14 kwa pointi 25 wakisaka pointi tatu ili kukwepa kushuka daraja.

Simba ndio mara ya kwanza msimu huu kucheza katika jiji la Mbeya baada ya mechi za awali kuwa Dar es Salaam, huku ikiweka historia pia kucheza saa 8 mchana kwa Ligi Kuu ikiwa ni mara ya kwanza.

Mwananchi imepita katika viunga vya uwanja wa Sokoine na kushuhudia mashabiki wengi wakiwa katika harakati za kukata tiketi kushuhudia mchezo huo.

Pia maeneo ya nje ya uwanja huo, shangwe, tambo na ngoma vilitawala huku jezi za Wekundu (nyekundu na nyeupe) zikiwa ndizo zinatesa zaidi.

Simba inakutana na wapinzani hao ikijivunia rekodi nzuri ya kushinda mechi nyingi zaidi kwani katika michezo 16 za mwisho, City imeambulia sare moja na kupoteza 15.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *