
Dar es Salaam. Tamko la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, la kutaka kuondolewa gereji, vyuma chakavu, vitu vya samani na kupakwa rangi kwa majengo yaliyopo kandokando ya barabara yanayoelezwa kuharibu sura ya jiji, limeonyesha sura mbili kwa wahusika.
Agizo la Chalamila ni muendelezo wa watangulizi wake waliowahi kutoa maagizo ya kuondoa gereji na watengenezaji wa vitu kandokando ya barabara kuu, wakisisitiza kuwa shughuli hizo husababisha msongamano, ajali na kuchafua miundombinu ya jiji.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, Oktoba 15, 2021, alipiga marufuku kile alichokiita “gereji bubu” na shughuli zote zilizokuwa zikifanyika katika hifadhi za barabara ili kulinda miundombinu na usafi.
Viongozi wengine ni Said Meck Sadiki na Paul Makonda, ambao nao walikuwa na mikakati tofauti, lakini yenye lengo moja la kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa safi, lenye mpangilio na linalovutia.
Baadhi ya wamiliki wa gereji jijini Dar es Salaam wamepongeza agizo la Chalamila la kuboresha usafi na mpangilio wa maeneo ya kazi, lakini wakasisitiza kuwa utekelezaji wake unapaswa kuzingatia hali halisi ya shughuli za sekta hiyo.
Wakizungumza na Mwananchi jana, Juni 16, na leo, Juni 17, 2026, wamiliki hao wamesema lengo la kuhakikisha jiji linakuwa safi ni jema, lakini sekta ya gereji kwa asili inahusisha uwepo wa magari yanayosubiri matengenezo, vipuri, mafuta na vifaa mbalimbali vya kazi, hali inayofanya iwe vigumu maeneo hayo kuonekana kama ofisi au maduka ya kawaida yenye mpangilio mkamilifu wa usafi.
“Wateja wanakuja kubadilisha oil, kufanya service au matengenezo mengine madogo. Akimaliza anaondoka. Magari mengi hayakai muda mrefu kama watu wanavyofikiria. Kazi yetu ni kutengeneza gari liondoke, si kulihifadhi,” amesema Haji Hussein wa Mabibo.
Kuhusu gereji, Hussein amesema Serikali ingeangalia zaidi magari yaliyotelekezwa barabarani au biashara zinazoziba njia badala ya kuyatazama maeneo ya gereji kwa mtazamo mmoja.
“Angesema magari yaliyopo barabarani yaondolewe au wanaoziba service road wachukuliwe hatua, hilo linaeleweka. Lakini sisi tupo pembezoni na hatuzuii shughuli za watu wengine,” amesema James Peter wa Ilala.
Ametolea mfano vipuri vinavyouzwa Tandale, wilayani Kinondoni, na kubainisha kwamba hiyo ndiyo biashara yao, lile gari linaloonekana bovu liko pale ili linunuliwe.
“Likiisha nunuliwa linaondoka, hiyo ndiyo biashara yao. Ukiwaondoa pale, kuna eneo mbadala watakwenda? Kama hakuna, maana yake umeua biashara yao.
“Hatukatai tunahitaji jiji liwe safi, lakini tuondolewe kwa utaratibu, si hivi tu. Tuko hapa nasi kutafuta riziki,” amesema na kuongeza.
“Watu wengi wanaona magari mabovu na vyuma chakavu, lakini hawajui hali halisi ya biashara hii. Wapo mafundi wanaofanya kazi katika maeneo madogo ya kupangisha. Ukiwaambia waondoke bila kuwawezesha, inaweza kuwa changamoto,” amesema.
Baadhi yao pia wameeeleza kuwa gereji nyingi zimekuwa zikifanya kazi katika maeneo hayo kwa miaka mingi na zimekuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa mafundi, vibarua, wauzaji wa vipuri, madalali wa magari na makundi mengine ya wananchi.
“Watu wanaona gereji tu, lakini hawaoni idadi ya watu wanaokula kupitia biashara hizi. Kuna mafundi, vibarua, wauzaji wa vipuri, wauza mafuta na madalali wa magari. Ukiondoa shughuli hizi bila mpango mbadala, kuna watu wengi watapoteza kipato,” amesema Nurdin Ally wa Ilala.
Ally amefafanua kuwa si mara ya kwanza viongozi kutoa maelekezo yanayohusu biashara za magari katika Jiji la Dar es Salaam.
“Wakati wa Mkuu wa Mkoa wa zamani, Paul Makonda, kulikuwa na maelekezo kuhusu showroom za magari (sehemu za kuuzia magari). Haya mambo si mapya.
“Tunachoomba ni mazungumzo na ufumbuzi unaozingatia maisha ya watu wanaotegemea sekta hii, lakini si kutoa maelekezo ndani ya mwezi mmoja. Sawa, tutatii sheria, lakini swali ni tutakwenda wapi na tutafanya nini baada ya hapo?” amehoji Nurdin.
Wauza vyuma chakavu
Wauza vyuma chakavu wa Tandale wamesema biashara yao mara nyingi huonekana kama uchafu, ilhali ni chanzo muhimu cha ajira na malighafi kwa viwanda mbalimbali.
Abdallah Khamis, amesema magari mabovu na vipuri vilivyotumika vinavyoonekana katika maeneo yao ni sehemu ya biashara inayowezesha urejelezaji wa bidhaa.
“Watu wanaona kama ni taka, lakini sisi tunaona mali. Kuna vipuri vinavyonunuliwa kila siku na vyuma vinavyopelekwa viwandani kwa ajili ya kuchakatwa upya. Kama Serikali inataka kuboresha mazingira, basi itusaidie kupata maeneo rasmi yenye miundombinu bora,” amesema Khamis.
Naye Asha Said, mfanyabiashara wa eneo hilo amesema sekta hiyo imeajiri vijana wengi ambao watakosa chanzo cha mapato iwapo biashara hizo zitaondolewa bila maandalizi.
Wauza samani
Mbali na wamiliki wa gereji, wafanyabiashara wa samani katika eneo la Mkwajuni, wilayani Kinondoni, nao wamesema wanaunga mkono juhudi za kuboresha mwonekano wa jiji, lakini wakataka utekelezaji wake uzingatie mazingira halisi ya biashara zao.
Mfanyabiashara wa vitanda, Salum Mushi, amesema biashara ya samani inahusisha kuonesha bidhaa nje ya maduka ili kuwavutia wateja, hivyo ni muhimu kuwe na mwongozo unaoeleweka badala ya kuondolewa ghafla.
“Mteja anapotafuta kitanda, sofa au kabati anatakiwa kuona bidhaa. Tunakubaliana na suala la usafi na mpangilio, lakini Serikali itoe maeneo au utaratibu unaotuwezesha kufanya biashara bila kuathiri mwonekano wa jiji,” amesema Mushi.
Wamiliki wa majengo
Baadhi ya wamiliki na wasimamizi wa majengo katikati ya Jiji la Dar es Salaam wamepokea kwa mtazamo chanya maelekezo ya kuboresha mwonekano wa majengo kwa kuyapaka rangi na kuyafanyia matengenezo ndani ya miezi mitatu.
Agizo kama hilo lilitolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, Septemba 8, 2025 aliyewataka wananchi kupaka rangi majengo yao, hususan katika maeneo ya Kariakoo, Mchikichini, Jangwani, Kivukoni, Kisutu, Gerezani, Mchafukoge, Upanga Mashariki na Upanga Magharibi.
Msimamizi wa jengo la Mtaa wa Mchikichi, eneo la Kariakoo, Hamis Mfaume, amesema changamoto iliyopo ni gharama za ukarabati na upakaji rangi, kwani majengo mengi ya zamani yanahitaji ukarabati mkubwa.
“Tunafahamu umuhimu wa majengo kuwa na mwonekano mzuri kwa wageni na wananchi. Changamoto iliyopo ni gharama za ukarabati na upakaji rangi ambazo, kwa baadhi ya majengo, ni kubwa. Hivyo tungependa kuona utaratibu unaowezesha utekelezaji kwa awamu,” amesema Mfaume.
Naye mmiliki wa jengo lililopo Mtaa wa Jamhuri, Rehema Mallya, amesema amri hiyo ya usafi wa majengo imetolewa mara ya pili, lakini kutotekelezwa kwake kuna changamoto. Hivyo, Serikali isiwe inaweka muda mfupi, kwani utakuwa chanzo cha msongo wa mawazo kwa watu kutafuta fedha na kuingia madeni.
“Tunaunga mkono wazo la kufanya Dar es Salaam ionekane ya kisasa zaidi, lakini ni muhimu mamlaka husika zikashirikisha wadau na kutoa muda wa kutosha ili kila mmoja aweze kutekeleza maelekezo hayo bila kuathiri shughuli zake za kiuchumi,” amesema Rehema.
Juhudi za viongozi wa mkoa
Viongozi mbalimbali waliowahi kuongoza Mkoa wa Dar es Salaam, akiwamo Amos Makalla, Said Meck Sadiki na Paul Makonda, wamekuwa na mikakati tofauti lakini yenye lengo moja la kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa safi, lenye mpangilio na linalovutia.
Kwa upande wake, Amos Makalla akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alifanya juhudi mbalimbali za kuboresha usafi na mpangilio wa jiji hilo kwa kutumia kampeni za uhamasishaji na usimamizi wa karibu.
Baadhi ya hatua zake kuu zilijumuisha kuhimiza siku za usafi wa pamoja, ambapo wananchi, taasisi na wafanyabiashara walishiriki kusafisha maeneo yao ya kazi na makazi.
Makalla aliongeza msukumo katika utekelezaji wa sheria za mazingira, ikiwemo kuwachukulia hatua wale wanaotupa taka ovyo, pamoja na kushirikiana na halmashauri kuboresha mifumo ya ukusanyaji na usafirishaji wa taka.
Kwa upande wake, Paul Makonda alijikita zaidi kwenye kampeni za usafi wa mara kwa mara, akihamasisha wananchi na taasisi kushiriki siku maalumu za usafi, pamoja na kuimarisha nidhamu ya usimamizi wa taka katika maeneo ya biashara na barabarani.
Pia, alisisitiza matumizi ya adhabu kwa wanaochafua mazingira kama njia ya kuleta mabadiliko ya tabia.
Kwa upande wake, Said Meck Sadiki alisisitiza dhana ya uwajibikaji wa pamoja, akieleza kuwa usafi si jukumu la Serikali pekee bali ni la kila mwananchi.
Alihimiza kampeni za usafi wa kila mwisho wa mwezi, pamoja na kutoa onyo kuhusu madhara ya uchafu katika kuvutia wawekezaji na kudhoofisha taswira ya jiji kimataifa.