
Akizungumza katika mkutano huo, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia Masuala ya Kibinadamu ambaye pia ni Mratibu wa Misaada ya Dharura, Tom Fletcher, amekumbusha kuwa Azimio la Baraza la Usalama namba 2803 (2025), lililopitishwa baada ya miezi kadhaa ya juhudi za upatanishi, limeleta mafanikio fulani. Amesema idadi ya vifo vya raia vilivyosababishwa na mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza imepungua, mateka waliokuwa wamechukuliwa na Hamas wakati wa mashambulizi ya Oktoba 7, 2023 wameachiliwa, na baadhi ya vikwazo vya utoaji wa misaada ya kibinadamu vimeondolewa.
Fletcher ameeleza kuwa miezi sita baada ya usitishaji vita kuanza kutekelezwa, Ukanda wa Gaza hauhesabiwi tena kuwa katika hali ya njaa ya kiwango kikubwa. Hata hivyo, amesisitiza kuwa hali bado ni mbaya sana.
Maendeleo madogo
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema Azimio 2803 pamoja na mpango uliopendekezwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, vilitarajiwa kuleta mabadiliko makubwa zaidi.
“Mafanikio haya dhaifu ndiyo kiwango cha chini kabisa cha kile ambacho Wapalestina wanahitaji, kile tunachoweza kutoa na kile ambacho sheria ya kimataifa inahitaji,” amesema Fletcher.
Kwa mujibu wake, hatua zilizopatikana zimeepusha tu hali mbaya zaidi, lakini hata mahitaji ya msingi ya wananchi bado hayajafikiwa.
Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, karibu Wapalestina 1,000 wameuawa tangu usitishaji vita utangazwe.
Mamilioni wanahitaji msaada
Fletcher pia amesema takribani asilimia 70 ya wakazi wa Gaza wanahitaji makazi, huku mfumo wa utoaji huduma ukiwa ukikaribia kuporomoka. Aidha, mpango wa kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu umepokea chini ya robo ya fedha zinazohitajika.
Ameitaka Baraza la Usalama kuhakikisha ulinzi wa raia, wakiwemo wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu, pamoja na kuruhusu misaada kufikishwa kwa usalama, bila vikwazo na katika maeneo yote ya Gaza. Pia amesisitiza umuhimu wa kutoa fedha zinazolingana na ukubwa wa mgogoro huo.
“Raia hawawezi kusubiri wakati mwafaka wa kidiplomasia ili wapate rasilimali wanazohitaji kuendelea kuishi,” amesisitiza Fletcher.
“Usitishaji vita haufanyi kazi”
Kwa upande wake, Mkuu wa Sera za Kibinadamu wa shirika la Oxfam International, Bushra Khalidi, amesema katika mkutano huo kuwa usitishaji vita hauleti matokeo yaliyotarajiwa.
“Usitishaji vita haufanyi kazi,” amesema Khalidi.
Ameeleza kuwa alikuwa akizungumza si tu kama afisa wa shirika la misaada, bali pia kama mama Mpalestina anayeishi Ukingo wa Magharibi. Amesema familia ya mume wake imekwama Gaza, huku mtoto wake akipitia maumivu ya kutengana na wapendwa wake pamoja na kulazimika kuhama makazi.
“Gaza inasambaratishwa tena. Watu wake wanaendelea kulazimishwa kujikusanya katika maeneo yanayozidi kupungua kwa kasi,” amesema.
Khalidi aliongeza kuwa raia bado wanalazimika kuhama makazi yao, wanakabiliwa na njaa na hawana ulinzi wa kutosha.
“Amani haiwezi kupimwa kwa matamko. Lazima ipimwe kwa nafasi ambayo watu wanayo kuishi maisha ya kawaida,” amesema.
Amefahamisha kuwa tangu Oktoba 2023, wafanyakazi wenzake pamoja na washirika wao wa Kipalestina wameweza kutoa msaada kwa karibu watu milioni 1.5 huko Gaza. Hata hivyo, miundombinu ya kibinadamu inayohitajika kwa ajili ya ujenzi na urejeshaji wa maisha imeharibiwa kwa makusudi, huku mashirika ya misaada yanayoaminika, ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina Mashariki ya Kati (UNRWA), yakizuiwa kutekeleza majukumu yao.
Khalidi amekumbusha kuwa Azimio 2803 lilipitishwa kwa lengo la kudumisha usitishaji vita na kushughulikia janga la kibinadamu la Gaza, lakini miezi saba baadaye hata malengo hayo ya msingi bado hayajatekelezwa kikamilifu.