Akizungumza leo kutokea Nairobi Kenya, msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, Seif Magango, amesema Umoja wa Mataifa unalaani vikali vurugu hizo ambazo ziliripotiwa kusababisha kifo cha angalau mtu mmoja na kujeruhi watu wasiopungua 38, wakiwemo viongozi wanne wa upinzani.

“Inasikitisha kwamba angalau mwandamanaji mmoja aliuawa na wengine wasiopungua 38 kujeruhiwa wakati wa maandamano hayo,” amesema Magango.

Serikali yatakiwa kulinda haki ya maandamano ya amani

Magango amekumbusha kuwa Serikali ya DRC ina wajibu wa kuwezesha mikusanyiko ya amani na kuhakikisha usalama wa washiriki wake. 

Amesisitiza kuwa matumizi yoyote ya nguvu na vyombo vya usalama yanapaswa kuwa hatua ya mwisho kabisa na yafanyike kwa kuzingatia kikamilifu sheria za kimataifa za haki za binadamu.

“Serikali ina wajibu wa kuwezesha maandamano ya amani na kulinda washiriki wake, huku matumizi ya nguvu yakibaki kuwa suluhu ya mwisho kabisa,” amesema.

Türk ataka uchunguzi huru kabla ya uchaguzi wa 2028

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, Volker Türk, amekaribisha tangazo la mamlaka za DRC kwamba zitachunguza tukio hilo, lakini amesisitiza umuhimu wa uchunguzi huo kuwa wa kina, huru, wazi na usio na upendeleo.

Amesema wale wote watakaobainika kuwajibika kwa ukiukwaji wa haki za binadamu wanapaswa kufikishwa mbele ya sheria kwa kuzingatia dhamana zote za haki ya kusikilizwa kwa haki.

“Uchunguzi lazima uwe huru, wa uwazi na usioegemea upande wowote, na wote watakaobainika kuwajibika wafikishwe mahakamani,” amesema Türk.

Aidha, Kamishna Mkuu huyo amezitaka mamlaka za DRC kuheshimu na kulinda kikamilifu uhuru wa kujieleza, kujumuika na kufanya mikusanyiko ya amani kuelekea uchaguzi wa urais na wabunge unaotarajiwa kufanyika mwaka 2028.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *