Kupitia ombi hilo lililotolewa leo mjini Roma, Italia, mashirika hayo yamesema El Niño inatarajiwa kuongezeka katika nusu ya pili ya mwaka 2026, ikileta ukame katika baadhi ya maeneo na mafuriko pamoja na dhoruba katika maeneo mengine. Hali hiyo inaweza kuathiri uzalishaji wa chakula, mifugo, upatikanaji wa maji na kuongeza hatari ya njaa kwa mamilioni ya watu.

FAO na WFP zimesema tayari zimejipanga kusaidia watu milioni 1.2, lakini ufadhili wa ziada wa dola milioni 167 utawezesha kuwafikia watu wengine milioni 7.6 na kufikisha jumla ya walengwa milioni 8.8.

Hatua za mapema ni mkombozi

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa FAO, Beth Bechdol, amesema hatua za mapema ni nafuu na zenye matokeo bora kuliko kusubiri janga litokee. Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WFP, Carl Skau, ameonya kuwa dunia haiwezi kumudu janga jingine la chakula, akisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua kabla madhara ya El Niño hayajawa makubwa.

Fedha hizo zitatumika kutoa misaada ya fedha taslimu, mbegu zinazostahimili ukame na mafuriko, kulinda mifugo, kuimarisha miundombinu ya maji na kutoa taarifa za tahadhari za mapema katika nchi zilizo hatarini.

Nchi zinazolengwa na mpango huo ni pamoja na Kenya, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Ethiopia, Uganda, Zimbabwe, Afghanistan, Pakistan, Ufilipino, Haiti, Guatemala, Honduras na Venezuela. 

Mashirika hayo yamesema mifumo na mipango ya utekelezaji tayari ipo, kinachohitajika sasa ni ufadhili wa haraka ili kuzuia madhara makubwa kabla hayajatokea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *