
Kupitia taarifa iliyotolewa leo jijini New York na msemaji wake Stéphane Dujarric, Katibu Mkuu amesema anasikitishwa zaidi na taarifa zinazoonesha kuwa kikosi cha Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kimepeleka nyongeza kubwa ya wanajeshi katika maeneo yanayozunguka El Obeid, hatua inayozua hofu ya uwezekano wa shambulio kubwa la ardhini dhidi ya mji huo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu, hali hiyo inaweza kuuweka mji wa El Obeid, ambao ni kitovu muhimu cha shughuli za kibinadamu katika eneo la Kordofan, katika hatari kubwa ya kushuhudia wimbi jipya la ghasia na umwagaji damu kwa kiwango kikubwa.
Ametoa wito kwa pande zote zinazohusika katika mzozo huo kujizuia na kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha raia wanalindwa. Amesisitiza kuwa mara nyingi katika mzozo huu, onyo la mapema limepuuzwa na kusababisha janga kubwa zaidi.
“Hatupaswi kuruhusu yaliyotokea El Fasher kujirudia tena El Obeid,” ameonya Katibu Mkuu, akitoa wito kwa wote wenye ushawishi kwa pande zinazopigana kutumia nafasi yao kuzuia kuongezeka kwa mapigano na umwagaji damu zaidi.
Katibu Mkuu pia amesisitiza tena wito wake wa kusitishwa mara moja kwa mapigano, akizitaka Jeshi la serikali ya Sudan (SAF) pamoja na Kikosi cha Msaada wa Harak RSF kushiriki katika juhudi za kimataifa za kutafuta suluhisho la kisiasa, ikiwemo juhudi zinazoongozwa na Mjumbe wake Maalum kwa Sudan.
Misaada ya kibinadamu
Wakati huo huo, mashirika ya kibinadamu yanaendelea kutoa msaada El Obeid na maeneo mengine ya Kordofan licha ya hali ya usalama kuzidi kuwa mbaya. Umoja wa Mataifa umesema mfanyakazi mmoja wa kibinadamu ni miongoni mwa raia waliouawa katika mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yaliyolenga maeneo ya makazi wiki hii.
Katibu Mkuu amesisitiza kuwa “wafanyakazi wa misaada na vifaa vya kibinadamu lazima viruhusiwe kusafiri kwa usalama bila vikwazo.” Aidha, raia wanaotaka kuondoka wanapaswa kuruhusiwa kufanya hivyo kwa usalama, huku wale wanaobaki wakihakikishiwa ulinzi na msaada wa kibinadamu wanaohitaji.
Mwisho, Katibu Mkuu amezikumbusha pande zote katika mzozo huo wajibu wao chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu, akisisitiza umuhimu wa kulinda raia, miundombinu ya kiraia, na kuhakikisha misaada ya kibinadamu inawafikia wahitaji kwa haraka, usalama na bila vikwazo.