
Huku akisema kuwa, nguvu ni matunda ya subira mitaani, medani ya vita na diplomasia kwa pamoja, Khatibu wa Swala ya Ijumaa ya mjini Tehran amesisitiza kuwa: ‘Leo utawala wa Marekani hauaminiki hata kidogo.’
Hujjatul Islam Walmuslimin Seyyed Mohammad Hassan Abu Torabifard amesema katika khutba zake za Swala ya Ijumaa mjini Tehran wiki hii kwamba: Subira ya pamoja ina maana ya kusimama imara mbele ya adui, kwa sababu Qurani Tukufu inasema subira yako haipasi kuwa ndogo kuliko ya adui. Subira ya taifa la Iran ndiyo iliyoishinda Marekani, na katika uwanja huu, subira ya taifa la Iran ilipita subira ya maadui wote na kupata ushindi wa mwisho.’
Ameashiria maneno ya George Bush, Rais wa zamani wa Marekani Septemba 1990, na mpango wake wa kubuni eti “utaratibu mpya wa dunia” na kusema: “Alizungumzia kuundwa kwa mfumo wa umoja baada ya kuporomoka Umoja wa Kisovieti na kudai kwamba ulimwengu unaoegemezwa kwenye misingi ya sheria, ustawi na heshima kwa mataifa yenye nguvu ulikuwa unaundwa. Lakini kiutendaji, muundo huo wa madaraka uliua shahidi mamia ya maelfu ya watu katika vita viwili vikubwa dhidi ya mataifa ya Iraq na Afghanistan, na kwa kutumia gharama ya takriban dola trilioni 5, ulifichua ukweli tofauti na utaratibu huo uliodaiwa. Leo, kivuli cha mfumo huu wa utawala wa mabavu dhidi ya ubinadamu, uadilifu na maadili ya kibinadamu kinaweza kuonekana wazi huko Gaza, Beirut, Palestina na Iran.”
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran ameendelea kusema: “Njia ya Imam Khamanei aliyeuawa shahidi karibuni nchini Iran ilikuwa nguvu kwa taifa la Iran na mhimili wa muqawama uliouwezesha kusimama imara dhidi ya Marekani na kutowaruhusu mabeberu wa dunia kupora maslahi ya mataifa huru. Nguvu hii iliundwa nchini Iran, na matunda yake yamekuwa mapambano dhidi ya mrengo wa kiburi wa kimataifa na mafanikio ya ushindi katika miaka ya hivi karibuni.”