Dar es Salaam. Wakili maarufu na mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda, Erias Lukwago, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na shitaka la kushindwa kuripoti madai ya njama za uhaini, hatua iliyozua mjadala mpya kuhusu uhuru wa kisiasa na haki za kisheria nchini humo.

Lukwago, ambaye ni miongoni mwa mawakili wanaomtetea kiongozi wa upinzani, Dk Kizza Besigye, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini Kampala akiwa ameonekana dhaifu kiafya baada ya kushikiliwa kwa siku kadhaa tangu alipokamatwa nyumbani kwake.

Dk Besigye, ambaye amewahi kugombea urais mara nne na kuwa mmoja wa wakosoaji wakubwa wa serikali ya Uganda, amekaa rumande kwa muda mrefu baada ya kukamatwa mwishoni mwa mwaka 2024 na kufikishwa katika mahakama ya kijeshi akikabiliwa na mashitaka ya uhaini na umiliki wa silaha.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na familia yake, Lukwago alikamatwa Juni 15 mwaka huu na watu wenye silaha wanaodaiwa kuwa maofisa wa usalama waliovamia makazi yake kabla ya kumpeleka kusikojulikana, bila kutoa maelezo rasmi kuhusu sababu za kukamatwa kwake.

Mahakama ilimsomea shitaka la kushindwa kutoa taarifa kuhusu njama inayodaiwa kuwa ya uhaini iliyopangwa kati ya mwaka 2021 na 2024, hatua iliyozua mjadala mpya kuhusu hali ya haki za binadamu na uhuru wa kisiasa nchini humo.

Waendesha mashtaka wameeleza kuwa kesi yake inahusishwa na uchunguzi wa madai ya uhaini unaomkabili Dk Besigye, ambaye Lukwago amekuwa akimwakilisha kisheria.

Kukamatwa kwake

Baada ya Lukwago kukamatwa makundi mbalimbali ya kisiasa na wanaharakati wa haki za binadamu yalipaza sauti hasa baada ya Mkuu wa Majeshi ya Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, kuandika ujumbe katika mitandao ya kijamii unaoonekana kuhusisha kukamatwa kwake.

Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, alichapisha picha zinazodaiwa kumuonyesha Lukwago akiwa amefungwa kitambaa machoni katika eneo lisilojulikana.

Pia, katika ujumbe mwingine, alieleza kuwa anajivunia hatua zilizochukuliwa dhidi ya mwanasiasa huyo, kauli ambazo zimezua ukosoaji kutoka kwa watetezi wa haki za binadamu.

Kwa upande wake kiongozi wa upinzani,  Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, amedai kuwa kukamatwa kwa Lukwago kulifanyika kwa maelekezo ya Kainerugaba wakati wakili huyo akijiandaa kuwasilisha hati ya mahakama dhidi ya mkuu huyo wa jeshi. Hata hivyo, madai hayo hayajathibitishwa na mamlaka za Uganda.

Kesi ya Lukwago imevuta hisia za wengi kutokana na nafasi yake kama wakili wa Dk Besigye, mwanasiasa mkongwe wa upinzani ambaye amekuwa akishikiliwa kwa tuhuma za uhaini tangu aliporejeshwa Uganda kutoka Kenya mwishoni mwa mwaka 2024 katika mazingira yaliyopingwa na mashirika mbalimbali ya haki za binadamu.

Besigye ni mmoja wa wapinzani wakubwa wa Rais Museveni. Kabla ya kuingia katika siasa za upinzani, aliwahi kuwa daktari binafsi wa rais huyo baadaye alitofautiana naye kisiasa mwaka 1999.

Tangu wakati huo, ameshiriki katika uchaguzi kadhaa wa urais dhidi ya Museveni na amekuwa akikamatwa mara kwa mara kutokana na shughuli zake za kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *