Kupitia taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataiafmchana huu wa Jumamosi Juni 20 saa za New York, Marekani, Baraza hilo pia limeeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuendelea kwa mapigano katika maeneo mbalimbali ya Sudan, hususan katika majimbo ya Kordofan, ambako ongezeko la mapigano linatishia kuzidisha zaidi hali mbaya ya kibinadamu ambayo tayari inaikabili nchi hiyo. Wajumbe wa Baraza walizitaka pande zote zinazohusika katika mzozo huo kusitisha mara moja mapigano ili kuzuia kuendelea kwa mateso ya raia.

Katika taarifa hiyo, Baraza la Usalama limekumbusha kuwa pande zote katika mzozo huo zina wajibu wa kuwalinda raia na kuheshimu sheria za kimataifa, ikiwemo sheria za kimataifa za kibinadamu, pamoja na kutekeleza ahadi zilizotolewa chini ya Azimio la Jeddah. Wajumbe pia wameeleza wasiwasi kuhusu taarifa za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yanayodaiwa kufanywa na RSF mjini El Obeid na kuongezeka kwa matumizi ya ndege hizo katika maeneo mengine ya Sudan. Baraza lilitaka ukiukwaji na unyanyasaji wote uchunguzwe na wahusika wawajibishwe.

Baraza la Usalama limesisitiza umuhimu wa kuruhusu misaada ya kibinadamu kufikishwa kwa usalama na bila vikwazo kwa watu wanaohitaji nchini Sudan. Wajumbe walizitaka pande zote kuruhusu raia kupita kwa usalama na kuwezesha mashirika ya misaada kufikia maeneo yaliyoathirika kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Aidha, wamezitaka nchi zote wanachama kuepuka kuingilia mzozo huo kwa namna inayoweza kuchochea vita na kuyumbisha juhudi za kufikia amani ya kudumu.

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamesisitiza tena dhamira yao ya kuunga mkono mamlaka, uhuru, umoja na ukamilifu wa eneo la Sudan. Pia wamekataa vikali juhudi zozote za kuanzisha mamlaka mbadala ya utawala katika maeneo yanayodhibitiwa na RSF. Baraza hilo limezitaka nchi zote kutekeleza wajibu wao chini ya sheria za kimataifa pamoja na kutekeleza maazimio husika ya Baraza la Usalama, ikiwemo Azimio namba 2791 la mwaka 2025, huku juhudi za kurejesha amani na utulivu nchini Sudan zikiendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *