Akiwa amezaliwa katika familia iliyokimbia mzozo nchini Sierra Leone na kujenga maisha mapya nchini Ujerumani, Rüdiger anasema mafanikio yake yametokana na fursa ambazo wazazi wake walipata baada ya kupata usalama.

Sasa akiwa anaiwakilisha Ujerumani katika Kombe la Dunia la FIFA 2026 na pia mwanachama wa Timu ya Gamechanging ya UNHCR, Rüdiger amesema safari ya familia yake imeunda mtazamo wake wa maisha. “Safari ya wazazi wangu iliwapeleka kutoka Sierra Leone hadi Ujerumani ambako walipata usalama dhidi ya mzozo na nafasi ya kujenga maisha bora kwa familia yetu. Kwa kweli, bila hilo, nisingekuwa hapa leo,” anaeleza.

Rüdiger anasema mchezo huo ulimpa hisia ya kuwa sehemu ya jamii na kumpa matumaini alipokuwa mtoto. “Soka siku zote limekuwa zaidi ya mchezo kwangu. Nilipokuwa mtoto, lilikuwa mahali nilipopata nafasi yangu, mahali pa matumaini na ndoto,” ameeleza, akiongeza kuwa michezo inaweza kuwasaidia vijana kurejesha matumaini na kuota maisha bora ya baadaye.

Anarudisha kwa jamii ‘nyumbani’

Leo, Rüdiger anawasaidia vijana nchini Sierra Leone kupitia taasisi yake, kwa kusaidia upatikanaji wa elimu, michezo na huduma za afya. Amesema athari za vita bado zinaonekana nchini humo na kwamba anataka kusaidia kuunda fursa kwa kizazi kipya.

“Kila ninachofanya kinarejea kwa wazazi wangu, safari yao na nguvu ya mchezo kubadilisha maisha,” amesema Rüdiger, akisisitiza kuwa wakimbizi wanaweza kustawi na kutoa mchango mkubwa kwa jamii wanapopewa usalama, msaada na nafasi ya kufanikiwa.

Viongozi wa Umoja wa Mataifa

Katika ujumbe wake mahususi wa siku hii, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Barham Ahmed Salih, ametoa pongezi kwa ujasiri na azma ya wakimbizi duniani kote, akisisitiza kwamba ingawa mtu anaweza kuwa mkimbizi kwa kipindi fulani, hali hiyo haipaswi kufafanua maisha yake yote. Amebainisha kuwa wakimbizi huchangia kwa kiasi kikubwa katika jamii zinazowapokea, wakifanya kazi kama wafanyakazi, wanafunzi, wafanyabiashara, wasanii na viongozi.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anatoa wito kama huo wa kuongezwa kwa msaada kwa wakimbizi na jamii zinazowahifadhi, ikiwa ni pamoja na kuheshimu sheria za kimataifa za wakimbizi, kulinda haki ya kuomba hifadhi, kuunda fursa za kujitegemea na kuongeza juhudi za kuleta amani. Katibu Mkuu pia anapongeza ukarimu wa nchi zinazoendelea ambazo zinahifadhi karibu robo tatu ya wakimbizi wote duniani, akihimiza dunia kushirikiana kulinda haki za watu waliolazimika kukimbia makazi yao kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *